Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa amewawasilishia wabunge wa mkoa wa Tanga taarifa ya tathmini ya awali ya kiwanda cha kusindika maziwa cha Tanga Fresh iliyofanywa na timu iliyoongozwa na Ofisi ya Mrajisi wa vyama vya ushirika nchini.
Akizungumza wakati wa kikao cha kuwasilisha tathamini hiyo kilichofanyika Juni 24,2026 Bungeni jijini Dodoma, Balozi Dkt. Bashiru amesema kuwa taarifa hiyo ni ya awali na haiwezi kutumika kufanya maamuzi yoyote kwa sasa mpaka taarifa ya Mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za Serikali itakapokamilika pia.
“Rai yangu ni kukamilika kwa haraka kwa uchunguzi huo na ni lazima uchunguzi huo ufike mpaka kwenye mzizi wake ili suluhu ya kudumu iweze kupatikana na rai yangu naomba tuendelee kuimarisha ushirika kwa sababu wafugaji wetu ni wadogo hivyo wanahitaji kuwa na mifumo ambayo kidogo kinachopatikana kitakuwa na usawa” Amesema Mhe. Balozi Dkt. Bashiru.
Kwa upande wa wabunge hao mbali na kumpongeza Balozi Dkt. Bashiru kwa jitihada zake za kuhakikisha kiwanda hicho kinarejea kwenye hadhi yake ya awali pamoja na hatua nyingine zitakazochukuliwa wameishauri Serikali kubadili muundo wa uendeshaji wa kiwanda hicho pindi taratibu za kiuchunguzi zitakapokamilika.
“Kile kiwanda ni alama ya mkoa wa Tanga na kila mmoja angetamani kuona kinafanya vizuri,wafugaji wengi wamepata mafanikio makubwa kupitia kile kiwanda na ndo sehemu pekee ambayo wafugaji walifahamu kiasi gani ushirika unalipa na wakawa na imani nao, nashauri mwisho wa uchunguzi pamoja na mambo mengine tubadilishe muundo wa uendeshaji wa kiwanda kile” Amesema Mhe. Rashid Shangazi ambaye pia ni mbunge wa jimbo la Mlalo mkoani Tanga.
Katika hatua nyingine Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa amemwelekeza Mratibu wa mradi wa Mageuzi ya tasnia ya maziwa na mabadiliko ya Tabia nchi kuandaa andiko rahisi linaloonesha namna mradi huo utakavyotekelezwa katika mikoa yote 8 ikiwa ni pamoja na mkoa wa Tanga na kuwakabidhi wabunge wa mikoa husika ili iwarahisishie kufikisha mradi huo kwa walengwa.




Hakuna maoni:
Chapisha Maoni