Breaking


Jumatano, 24 Juni 2026

TWPF YAKAGUA MRADI WA KIMKAKATI DODOMA




BODI ya Mfuko wa Kuhifadhi Wanyawapori (TWPF) imetembelea kiwanja kinachomilikiwa na Mfuko wa Kuhifadhi Wanyamapori Tanzania lililopo katika eneo la Njedengwa, Jijini Dodoma 

Msafara wa Bodi hiyo umeongozwa na Mwenyekiti wake, Profesa Jafari Kideghesho akiambatana na Katibu wa Bodi hiyo ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Alexander L. Lobora na wajumbe wengine wa Bodi.

Wajumbe hao ni Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI) Dkt. Eblate E. Mjingo na Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) Mlage Kabange na Victoria Shayo akimwakilisha Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro.

Akizungumza baada ya kukagua kiwanja hicho chenye ukubwa wa mita za mraba 39,700, Profesa Kideghesho amesema ameridhishwa na usimamizi na uhifadhi wa kiwanja hicho na kuwaelekeza wajumbe wa Skretarieti ya TWPF kujipanga katika kuandaa mipango ya kuendeleza kiwanja hicho katika shughuli za uwekezaji wa kimkakati.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, Dkt. Alexander L. Lobora amesema Mfuko utalitumia eneo hilo kama eneo la kimkakati la uendeshaji wa shughuli za kutunisha mapato ya Mfuko.

Mfuko wa Hifadhi ya Wanyamapori Tanzania uko kisheria kwa ajili ya kuwezesha shughuli zinazohusiana na uhifadhi wanyamapori ndani na nje ya maeneo yaliyohifadhiwa ambazo kwa kawaida huhitaji fedha nyingi.

Hakuna maoni: