Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo anayeshughulikia Utafiti, Profesa Nelson Boniface, alisema maadhimisho hayo yatajadili nafasi ya utafiti na ubunifu katika kuongeza thamani ya rasilimali mbalimbali za Tanzania, ikiwemo sekta ya madini, ili kuchangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs).
Profesa Boniface alibainisha kuwa Tanzania ina utajiri mkubwa wa rasilimali za asili ambao unaweza kuwanufaisha wananchi zaidi kupitia tafiti na ubunifu unaolenga kuongeza thamani ya bidhaa na huduma zinazotokana na rasilimali hizo.
Maadhimisho hayo yatajumuisha mihadhara ya kitaaluma, makongamano, mijadala ya kitaalamu pamoja na majukwaa ya kujenga ushirikiano kati ya vyuo vikuu, taasisi za utafiti, sekta binafsi, viwanda na Serikali.
“Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kinawahimiza wananchi, wanafunzi, watafiti na wadau wa maendeleo kushiriki kikamilifu katika maadhimisho haya ambayo ni jukwaa muhimu la kuonesha mchango wa utafiti na ubunifu katika kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini,” alisema Profesa Boniface.
Kwa upande wao, Mkurugenzi wa Ubunifu na Ujasiriamali wa UDSM, Profesa Lilian Kaale, pamoja na Mkurugenzi wa Utafiti na Machapisho, Dk. Mathew Senga, walisema chuo hicho kinaendelea kuweka mkazo katika kuhakikisha matokeo ya tafiti na bunifu yanawafikia walengwa na kuleta manufaa ya moja kwa moja kwa jamii.
Ufunguzi rasmi wa Maadhimisho ya Wiki ya 11 ya Utafiti na Ubunifu unatarajiwa kufanywa na Anthony Mavunde, huku hafla ya kufunga ikitarajiwa kuongozwa na Caroline Nombo.
UMUHIMU WA MAADHIMISHO
Wiki ya Utafiti na Ubunifu ya UDSM imekuwa jukwaa muhimu la kuunganisha watafiti, wabunifu, wanafunzi na wadau mbalimbali kwa lengo la kuhamasisha matumizi ya maarifa na teknolojia katika kutatua changamoto za maendeleo na kuimarisha uchumi wa Tanzania.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni