Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na wizara hiyo kupitia mtandao wa X, visa vipya viligunduliwa miongoni mwa watu waliokuwa na mawasiliano ya karibu na wagonjwa waliothibitishwa awali kuwa na ugonjwa huo.
Uganda iliripoti kisa chake cha kwanza cha Ebola mnamo Mei 15, baada ya kifo cha raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) aliyekuwa akipatiwa matibabu katika hospitali binafsi nchini humo. Tangu wakati huo, maambukizi mengine yameendelea kuripotiwa, yakiwemo baadhi ya visa vilivyowahusisha wahudumu wa afya.
Katika juhudi za kudhibiti kuenea kwa ugonjwa huo, Wizara ya Afya imesema kuwa kwa sasa inafuatilia watu 668 waliokuwa karibu na wagonjwa waliothibitishwa kuwa na Ebola. Ufuatiliaji huo ni sehemu ya mikakati ya kuzuia maambukizi mapya na kubaini mapema watu wanaoweza kuwa katika hatari.
Wakati huohuo, mamlaka za afya nchini Uganda zimetangaza habari njema baada ya wagonjwa wawili wa Ebola kuruhusiwa kutoka hospitalini kufuatia kupona kabisa ugonjwa huo.
UGANDA KUWA MWENYEJI WA KITUO CHA KIKANDA CHA AFRICA CDC
Mbali na juhudi za kukabiliana na mlipuko wa Ebola, Uganda inatarajiwa kuwa mwenyeji wa Kituo cha Kikanda cha Kukabiliana na Majanga ya Magonjwa chini ya taasisi ya Africa Centres for Disease Control and Prevention (Africa CDC).
Kituo hicho kitakuwa na jukumu la kuimarisha ufuatiliaji wa magonjwa, kuratibu hatua za kukabiliana na milipuko, kutoa msaada wa maabara, kuimarisha maandalizi ya dharura za afya ya umma, kufanya tafiti pamoja na kupeleka wataalamu wa afya katika maeneo yanayokumbwa na dharura za kiafya.
Wataalamu wa afya wanaamini kuwa uwepo wa kituo hicho utachangia kuimarisha uwezo wa nchi za Afrika Mashariki na Kati katika kukabiliana na milipuko ya magonjwa hatari kama Ebola na magonjwa mengine ya kuambukiza.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni