Breaking


Jumanne, 2 Juni 2026

WANAFUNZI 750 WA VYUO VIKUU WAELIMISHWA MATUMIZI YA MFUMO WA IDRAS

 

Takribani wanafunzi 750 kutoka vyuo mbalimbali vya elimu ya juu wamepatiwa mafunzo kuhusu matumizi ya Mfumo wa Integrated Domestic Revenue Administration System (IDRAS) katika jitihada za kuongeza uelewa wa masuala ya kodi na matumizi ya mifumo ya kidijitali nchini.

Mafunzo hayo yalitolewa na Maafisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katika Chuo cha Uhasibu Tanzania (TIA), yakihusisha wanafunzi kutoka vyuo vya TIA, CBE, IFM, CFR na MNMA.

Kupitia mafunzo hayo, wanafunzi walijifunza namna ya kutumia mfumo wa IDRAS, umuhimu wake katika usimamizi wa kodi, pamoja na mchango wake katika kuboresha utoaji wa huduma za kodi kwa wananchi na wadau mbalimbali nchini.

TRA imeeleza kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya mkakati wake wa kuendelea kusambaza elimu ya kodi kwa makundi tofauti ya jamii, hususan vijana na wanafunzi wa vyuo vikuu ambao ni sehemu muhimu ya nguvu kazi na walipa kodi wa baadaye.

Aidha, mfumo wa IDRAS umeendelea kuwa nyenzo muhimu katika kuimarisha usimamizi wa mapato ya Serikali kwa kuwezesha utoaji wa huduma za kodi kwa njia ya kidijitali, kuongeza uwazi na kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa walipa kodi.

Jitihada hizi zinaonesha dhamira ya TRA ya kuhamasisha matumizi ya teknolojia katika sekta ya kodi na kuwajengea wananchi uelewa unaohitajika ili kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya uchumi wa taifa.


Hakuna maoni: