Breaking


Alhamisi, 11 Juni 2026

WAZIRI NDEJEMBI AZINDUA KITUO CHA KUCHAJIA VYOMBO VYA USAFIRI VYA UMEME DODOMA


Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, amezindua rasmi Kituo cha Kuchajia Vyombo vya Usafiri Vinavyotumia Umeme katika Ofisi za Shirika la Umeme Tanzania, TANESCO, jijini Dodoma, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali kuhamasisha matumizi ya nishati safi na teknolojia rafiki kwa mazingira.

Uzinduzi huo umefanyika Juni 11, 2026 sambamba na utiaji saini na uzinduzi wa miradi mbalimbali ya nishati safi, ikiwemo Mradi wa Ujenzi wa Vituo vya Kuchajia Vyombo vya Usafiri Vinavyotumia Umeme (EV Charging Stations) pamoja na Mpango wa Ukopeshaji wa Majiko ya Umeme kwa Wateja wa TANESCO (On-Bill Financing – OBF). Hafla hiyo imefanyika katika Viwanja vya Mashujaa, Jamatini, jijini Dodoma.


Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Ndejembi amesema miradi hiyo ni hatua muhimu katika kuimarisha matumizi ya umeme nchini, huku ikichangia kupunguza utegemezi wa nishati zinazochafua mazingira na kuongeza ufanisi katika sekta ya usafirishaji na matumizi ya kupikia.


Kwa mujibu wa TANESCO, ujenzi wa vituo vya kuchajia magari ya umeme unalenga kuandaa mazingira bora kwa ukuaji wa teknolojia ya usafiri wa kisasa nchini, wakati mpango wa ukopeshaji wa majiko ya umeme ukitarajiwa kuongeza matumizi ya nishati safi majumbani kwa kuwapa wananchi fursa ya kupata vifaa hivyo kwa urahisi.


Serikali imeeleza kuwa utekelezaji wa miradi hiyo utaendelea kusaidia kuboresha maisha ya wananchi kupitia upatikanaji wa nishati ya umeme iliyo nafuu, salama na yenye ufanisi, sambamba na kuchochea maendeleo ya uchumi na kulinda mazingira kwa vizazi vya sasa na vijavyo.


Hakuna maoni: