Breaking


Ijumaa, 17 Julai 2026

LAMINE YAMAL AWATOA HOFU KABLA YA FAINALI

 Mshambuliaji kijana wa Hispania, Lamine Yamal, ameripotiwa kutofanya mazoezi na kikosi chake kutokana na kuhisi maumivu madogo ya misuli kwenye paja.

Kwa mujibu wa taarifa zilizoripotiwa na Marca na kunukuliwa na mwandishi wa masuala ya usajili Fabrizio Romano, Yamal alionekana akiwa amefungwa bandeji kwenye eneo la paja wakati wa mazoezi. Hata hivyo, taarifa hizo zinaeleza kuwa hali yake si ya kutia wasiwasi na hayuko katika hatari ya kuukosa mchezo wa fainali ya Kombe la Dunia.

Mipango ya benchi la ufundi la Hispania inaelezwa kuwa ni kumuanza nyota huyo mwenye umri mdogo katika kikosi cha kwanza kwenye mchezo huo mkubwa utakaopigwa Jumapili jijini New York, Marekani.


Iwapo ataanza kama ilivyopangwa, Yamal atakutana uso kwa uso na nahodha wa Argentina,
Lionel Messi, katika moja ya mechi zinazosubiriwa kwa hamu zaidi na mashabiki wa soka duniani. Mchezo huo unatazamwa kama pambano la kizazi kipya dhidi ya mmoja wa wachezaji bora zaidi kuwahi kucheza mchezo huo.

Licha ya usumbufu huo wa misuli, hakuna taarifa rasmi zinazoonyesha kuwa Yamal atakosekana kwenye kikosi. Timu ya madaktari inaendelea kufuatilia maendeleo yake huku matarajio yakiwa ni kuhakikisha yuko katika hali nzuri ya kuisaidia Hispania kwenye fainali hiyo muhimu.

Mashabiki wa soka duniani sasa wanasubiri kuona ikiwa nyota huyo chipukizi ataendelea kung’ara dhidi ya Messi katika mchezo unaotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa na kuandika historia mpya ya Kombe la Dunia.


Hakuna maoni: