Breaking


Alhamisi, 30 Julai 2026

MKUTANO WA TUME YA PAMOJA YA KUDUMU KATI YA TANZANIA NA ANGOLA WAANZA JIJINI LUANDA


Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa, ameshiriki Mkutano wa Tatu wa Tume ya Pamoja ya Kudumu (Joint Permanent Commission - JPC) kati ya Tanzania na Angola unaofanyika jijini Luanda kwa siku mbili, kuanzia Julai 29 hadi 30, 2026.

Mkutano huo umeanza katika ngazi ya Maafisa Waandamizi, ambapo wajumbe kutoka Tanzania na Angola wamejadili utekelezaji wa maazimio yaliyofikiwa katika mkutano uliopita wa JPC uliofanyika Zanzibar mwaka 2024. Aidha, pande hizo mbili zimeweka mikakati mipya ya kuimarisha ushirikiano kwa manufaa ya mataifa yote mawili.

Akizungumza wakati wa kufunga mkutano wa ngazi ya Maafisa Waandamizi, Balozi Said Shaib Mussa amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha kuwa maazimio yote yatakayofikiwa katika mkutano huo yanatekelezwa kwa ufanisi ili kuleta matokeo chanya kwa wananchi wa Tanzania na Angola.


Kupitia Tume hiyo ya Pamoja ya Kudumu, Tanzania na Angola zinatarajia kuimarisha zaidi uhusiano wa kidiplomasia na kupanua ushirikiano katika sekta mbalimbali, zikiwemo diplomasia, ulinzi na usalama, biashara na uwekezaji, maendeleo ya jamii, afya, elimu, sayansi, teknolojia pamoja na ubunifu.

Mkutano wa ngazi ya Mawaziri unatarajiwa kufanyika Julai 30, 2026, ambapo mawaziri kutoka pande zote mbili watapokea na kujadili taarifa ya wataalamu, kupitisha maazimio ya Mkutano wa Tatu wa JPC, na kuweka mwelekeo wa utekelezaji wa maeneo mapya ya ushirikiano kati ya Tanzania na Angola.

Mkutano huu unatarajiwa kuendelea kuimarisha uhusiano wa kihistoria kati ya Tanzania na Angola, huku ukifungua fursa mpya za ushirikiano wa kiuchumi, kijamii na kisayansi kwa manufaa ya mataifa yote mawili.


Hakuna maoni: