Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Masafa Early Childhood Foundation, Dorice Kaijage, wakati wa kikao cha tathmini ya utekelezaji wa programu hiyo kilichofanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam. Kikao hicho kililenga kutathmini hatua zilizofikiwa tangu kuanza kwa programu, kubaini changamoto zilizojitokeza na kujadili njia bora za kuzitatua ili kuongeza ufanisi wa utekelezaji wake.
Kaijage amesema programu hiyo ilianza kutekelezwa mwaka 2021 na inatarajiwa kukamilika mwezi Septemba 2026. Kwa kipindi hicho, taasisi hiyo imefanikiwa kushirikiana na Serikali pamoja na wadau wengine katika kuanzisha na kuimarisha vituo vya huduma kwa watoto katika maeneo mbalimbali, ikiwemo Mbagala Zakhem, Soko la Magomeni na Kibada, Kigamboni.Ameeleza kuwa lengo kuu la vituo hivyo ni kuhakikisha watoto wanapata huduma muhimu zinazochangia maendeleo yao ya awali, ikiwemo elimu ya awali, huduma za afya, fursa za kujifunza, malezi yenye mwitikio kutoka kwa wazazi na walezi, pamoja na ulinzi na usalama wa mtoto.
Kwa mujibu wa Kaijage, mwitikio wa wazazi na walezi umekuwa wa kuridhisha, ambapo wengi wameendelea kuwapeleka watoto wao kwenye vituo vya afya na shule. Aidha, elimu kuhusu malezi bora imeendelea kutolewa kupitia mitandao ya kijamii, kampeni za nyumba kwa nyumba na ushirikiano na viongozi wa dini ili kuongeza uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa uwekezaji katika maendeleo ya mtoto tangu akiwa mdogo.
Kikao hicho cha tathmini kilihusisha wawakilishi kutoka Halmashauri za Kinondoni, Jiji la Dar es Salaam, Ubungo, Temeke na Kigamboni. Pia kilihudhuriwa na wadau wa maendeleo ya mtoto, Dawati la Jinsia pamoja na maafisa lishe, ambao walijadili namna ya kuimarisha ushirikiano katika utekelezaji wa programu hiyo.
Wadau walisisitiza umuhimu wa kuendelea kushirikiana ili kuhakikisha kila mtoto anapata haki zake za msingi na mazingira bora yatakayomwezesha kufikia uwezo wake kamili katika hatua za awali za maisha.












Hakuna maoni:
Chapisha Maoni