Breaking


Ijumaa, 18 Septemba 2026

KAMPUNI BINAFSI ZA ULINZI ZATAKIWA KUSALIMISHA SILAHA HARAMU KWA HIARI.



Kampuni binafsi za ulinzi zinazomiliki silaha bila kuwa na vibali halali zimetakiwa kuzisalimisha kwa hiari katika Jeshi la Polisi na kufuata taratibu zilizowekwa ili kupata vibali na kuzimiliki kihalali.

Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Patrobas Katambi, Kamishna wa Polisi Jamii, CP Alex Mkama, amewataka wakurugenzi na wamiliki wa kampuni binafsi za ulinzi kuhakikisha wanaendesha shughuli zao kwa kuzingatia kikamilifu sheria, taratibu na masharti yaliyowekwa katika kumiliki, kuhifadhi na kutumia silaha kwa ajili ya shughuli za ulinzi.

CP Mkama ameyasema hayo Septemba 18, 2026, mkoani Dodoma, wakati akizungumza na wakurugenzi na wamiliki wa kampuni 113 za ulinzi walioshiriki Mkutano wa Nne wa Umoja wa Kampuni Binafsi za Ulinzi Tanzania (UKUTA).


Aidha, amewataka wakurugenzi na wamiliki wa kampuni hizo kuhakikisha askari wanaokabidhiwa silaha wanapatiwa mafunzo stahiki na kuwa na uelewa wa kutosha kuhusu matumizi salama na sahihi ya silaha, pamoja na kuzingatia wajibu na taratibu za kiusalama wakati wote wanapotekeleza majukumu yao.


CP Mkama amesisitiza kuwa kampuni binafsi za ulinzi zina nafasi muhimu katika kulinda raia na mali zao, hivyo zinapaswa kutekeleza majukumu yao kwa weledi, nidhamu na kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa. 

Hakuna maoni: