Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Dkt. Jabiri Bakari, ni miongoni mwa Wakurugenzi Wakuu wa Taasisi za Muungano waliohudhuria kikao cha Wakuu wa Taasisi za Muungano kilichofunguliwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius John Ndejembi, Septemba 19, 2026, katika Ukumbi wa Golden Tulip, Zanzibar. Mhe. Makamu wa Rais kupitia kikao hicho amesisitiza juu ya umuhimu wa taasisi hizo za Muungano kuwaelimisha wananchi wanachokifanya na umuhimu wake.
Makamu wa Rais amezitaka Taasisi za Muungano kuimarisha ushirikiano, kubaini na kutumia fursa zilizopo pamoja na kushiriki kwa pamoja katika shughuli mbalimbali ndani na nje ya nchi kwa lengo la kuongeza tija na kuleta manufaa zaidi kwa Watanzania. Amesema viongozi wa taasisi hizo wanapaswa kuelewa kwa kina wajibu wao wa kuwahudumia wananchi na kufanya kazi kwa mtazamo mmoja wa kujenga “nyumba moja”, huku maslahi ya Watanzania yakiwekwa mbele. Aidha, amesema matarajio ya wananchi ni kuona Muungano na taasisi zake zikitoa matokeo yanayogusa maisha yao moja kwa moja, hususan katika uchumi, afya, elimu na maeneo mengine muhimu ya kijamii.
Mhe. Ndejembi amezihimiza taasisi hizo kuondoa vikwazo vinavyoweza kudhoofisha ushirikiano na kutumia fursa zilizopo katika pande zote mbili za Muungano ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao.
Akizungumza kabla ya kumkaribisha Makamu wa Rais, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, amesema kikao hicho kinalenga kuimarisha ushirikiano kati ya Taasisi za Muungano na Ofisi ya Makamu wa Rais, kuongeza uelewa wa pamoja kuhusu masuala ya Muungano na majukumu ya taasisi hizo, pamoja na kuweka mwelekeo wa kuimarisha utendaji na kuongeza ufanisi. Kikao hicho kimehudhuriwa na wakuu wa Taasisi 39 za Muungano, akiwemo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Mhe. Hamza Hassan Juma, Makatibu Wakuu na Watendaji Wakuu wa Taasisi, ambao wamepata fursa ya kujadili namna ya kuimarisha uratibu, kubadilishana uzoefu na kuweka mikakati ya pamoja kwa manufaa ya wananchi.



Hakuna maoni:
Chapisha Maoni