Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Ng’wasi Damas Kamani, ameitaka Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) kuendelea kufanya tafiti kuhusu athari zinazoweza kusababishwa na mvua za El Niño katika uzalishaji sekta ya uvuvi, ili kuwezesha serikali na wadau kuchukua hatua stahiki kukabiliana na changamoto hizo.
Mhe. Kamani ameyasema hayo leo, Septemba 12, 2026, jijini Mwanza, wakati wa ziara maalum ya kikazi ya siku tatu yenye lengo la kufuatilia utekelezaji wa maelekezo yaliyotolewa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, kwa Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA) Kampasi ya Nyegezi, pamoja na Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) Mwanza, ziara ambayo pia inalenga kuzungumza na vijana wanaoshiriki katika mpango wa Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT) – Uvuvi.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mhe. Kamani amesema TAFIRI inapaswa kufanya utafiti wa kina ili kubaini athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua za El Niño, hususan kwa wawekezaji, uzalishaji wa samaki na wadau wengine wa Sekta ya Uvuvi.
“Nataka mfanye utafiti wa athari zinazoweza kujitokeza wakati wa mvua za El Niño ili kuweza kuchukua hatua stahiki katika kupambana na athari zinazoweza kuwakumba wawekezaji katika Sekta ya Uvuvi, pia muangalie samaki wataathirika kwa kiasi gani ili kuzuia madhara hayo na kuweza kutoa elimu kwa wadau wa Sekta,” amesema Mhe. Kamani.
Aidha, Mhe. Kamani ameitaka Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA) kuhakikisha inajenga na kuboresha miundombinu ya vyumba vya ubaridi kwa ajili ya kuhifadhia samaki katika vituo vyake vya Kagara, Mara, Chato na Nyegezi, hatua ambayo itasaidia vijana wanaonufaika na mpango wa Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT) – Uvuvi, pamoja na wadau wengine, kuwa na uwezo wa kuhifadhi samaki baada ya kuvuna na hivyo kupunguza upotevu wa mazao ya uvuvi.
Pia, Naibu Waziri ameitaka FETA kushughulikia changamoto ya ulishaji wa samaki kupita kiasi, akisisitiza umuhimu wa vijana kufuata maelekezo ya kitaalamu kuhusu kiwango sahihi cha chakula kinachopaswa kutolewa kwa samaki.
Vilevile, ameitaka FETA kuendelea kuwasimamia na kuwahamasisha vijana wa BBT ili kila wanapovuna mazao ya uvuvi, watumie sehemu ya mapato yao kuongeza vizimba vya ufugaji wa samaki, ambapo ameweka bayana kuwa kufanya hivyo kutawawezesha vijana kuongeza uzalishaji, kukuza shughuli zao za uvuvi na ufugaji wa samaki pamoja na kuongeza kipato na kujenga maisha bora.
Mhe. Kamani amewapongeza vijana wa BBT kwa kujituma katika shughuli za Uzalishaji na kuwataka waenndelee kutumia vizuri fursa walizopata na fursa zinazoendelea kutolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuweza vijana kwa kupata mikopo ili kuinua vipato vyao na kupambana na changamoto za ajira.






Hakuna maoni:
Chapisha Maoni