

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limetoa tahadhari kwa wananchi kuhusu kuchukua hatua za kuzuia madhara yanayoweza kujitokeza kutokana na athari za El Niño, ikiwemo mafuriko na uharibifu wa mazingira.
NEMC imewataka wananchi kuepuka kutiririsha maji machafu kwenye mikondo ya maji, mito na vyanzo vya maji, pamoja na kusafisha mifereji na kuhakikisha taka hazizuii njia za maji.
Aidha, wananchi wamehimizwa kulinda maeneo oevu na kingo za mito, kuzuia mmomonyoko wa udongo na kutunza uoto wa asili ili kupunguza madhara yanayoweza kusababishwa na mvua kubwa.
Baraza hilo pia limewataka wananchi wanaoishi katika maeneo ya mabondeni kuchukua tahadhari kwa kuhama na kwenda maeneo salama, huku wakikumbushwa kutotupa taka kwenye mifereji, mito na maeneo ya wazi.
NEMC imewahimiza wananchi kuchukua hatua mapema kwa ajili ya kulinda mazingira na usalama wa jamii, ikiwa ni sehemu ya kaulimbiu yake isemayo: “Mazingira Yetu, Uhai Wetu; Tuyatunze, Yatutunze.”
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni