Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar Mhe.Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha adhma na maono hayo ya Dira, Ilani na Mipango mbalimbali ya maendeleo yanafikiwa kama inavyotarajiwa.
Mhe. Dkt. Mwinyi ameyasema hayo katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa kituo cha mafunzo, elimu na michezo Jimbo la Kikwajuni, Zanzibar, Septemba 19, 2026 akieleza kuwa Serikali inatekeleza maono hayo kwa kushirikiana na Taasisi mbalimbali za Binafsi na Umma.
“Leo hii nimeshiriki uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa Kituo cha Kisasa cha Mafunzo, Elimu na Michezo kwa Vijana ambacho kama tulivyojulishwa ni mradi ambao umebuniwa na kutekelezwa na TAYI.
TAYI ni Taasisi inayofikia takribani miaka 15 tokea kuanzishwa kwake na imesaidia vijana wengi kubadilisha mitazano na maisha yao kupitia fani mbalimbali za mafunzo zilizokuwa zikitolewa katika kituo hiki ikiwemo michezo, ujasiriamali, ubunifu, mitindo, sanaa, ufundi, lugha, teknolojia ya habari, kompyuta, mazingira na ulinzi shirikishi.
Amesema utekelezaji wa mradi huo ni hatua muhimu ya ushirikiano baina ya Serikali na Sekta binafsi katika kuyafikia malengo ya Dira yetu ya maendeleo ya 2050. Akieleza kuwa mradi huo utakapokamilika unatarajiwa Kuongeza ajira kwa vijana; Kupanua fursa za Biashara na Ujasiriamali; na Kujenga jamii imara na bunifu kupitia mafunzo mbalimbali yatakayotolewa.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Kikwajuni ambaye ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni amesema Tanzania inaendelea na utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Zanzibar ya mwaka 2050 ambayo inalenga kuleta mabadiliko makubwa ya kiuchumi na kijamii kwa kuimarisha msingi wa rasilimali watu wenye afya, ushindani, ubunifu na tija.
Amesema tangu kuanzishwa kwake TAYI imefanikiwa kuleta mabadiliko kwa vijana wengi waliopata fursa ya kupata taaluma mbalimbali zilizotolewa Kituoni hapo ambapo inakadiliwa kuwa wanafunzi 1800 wamepita na kupata mafunzo mbalimbali TAYI.
“TAYI inaamini kwamba maendeleo ya vijana hayawezi kufikiwa na taasisi moja pekee. Kwa msingi huo, tunaendelea kuimarisha ushirikiano na Serikali, taasisi za elimu, sekta binafsi, mashirika ya maendeleo na jamii.” Amesema Mhe. Masauni.
Mhe. Masauni amesema katika kipindi cha Uongozi wa Mhe. Dkt. Mwinyi umeendelea kuacha alama, Taasisi ya TAYI ikizidi kuimarika na kufikia malengo ya kufanya kuwa kituo bora chenye kutoa majawabu na suluhisho ya mahitaji ya vijana sio tu Zanzibar na Tanzania Bara bali Afrika Mashariki na kati kwa ujumla.






Hakuna maoni:
Chapisha Maoni