Breaking


Jumatano, 16 Septemba 2026

TASAC KAGERA YAWAELEKEZA WADAU BUKOBA KUZINGATIA TAARIFA ZA HALI YA HEWA

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), kupitia Ofisi ya Mkoa wa Kagera, limewaelekeza wadau wa usafiri majini katika maeneo ya Bukoba kuzingatia taarifa rasmi za hali ya hewa zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), kufuatia matarajio ya mvua za Vuli zinazoanza katika wiki ya nne ya Septemba hadi Desemba 2026 na ambazo zinatarajiwa kuathiriwa kwa kiwango kikubwa na El Niño.

Afisa Mfawidhi wa TASAC Mkoa wa Kagera, Nahodha Mzee Mvihanga, ameyasema hayo alipotembelea na kufanya mikutano ya uhamasishaji katika Bandari za Kemondo na Bukoba, ambapo alitoa elimu kwa wadau kuhusu tahadhari muhimu za kuzingatia wakati wa msimu huo.

Nahodha Mvihanga amesema kuwa taarifa za hali ya hewa ni muhimu katika kufanya maamuzi salama ya safari za majini, hasa kutokana na uwezekano wa kutokea kwa mvua kubwa na upepo mkali, hali inayoweza kuongeza hatari kwa wavuvi, abiria na waendeshaji wa vyombo vya usafiri majini.

Amesema kila mmiliki na mwendeshaji wa chombo anapaswa kuhakikisha chombo kimesajiliwa na TASAC, kina cheti halali pamoja na vifaa muhimu vya usalama, hususan jaketi okozi za kutosha, na kuhakikisha vinatumika ipasavyo.

“Ni muhimu kwa kila anayefanya kazi katika chombo kuhakikisha chombo kimesajiliwa na TASAC na kina cheti halali ambacho hakijaisha muda wake. Vilevile, chombo kiwe na jaketi okozi za kutosha na watumiaji wazivae wakati wote wanapokuwa safarini,” alisema Nahodha Mzee Mvihanga.

Lengo la uhamasishaji huo ni kutoa tahadhari kwa umma, hususan wavuvi, wamiliki na waendeshaji wa vyombo vya usafiri majini, mabaharia, abiria na wadau wengine, ili wachukue tahadhari stahiki na kuepuka safari endapo hali ya hewa si salama.

TASAC imeendelea kuwasihi wadau kufuatilia taarifa za TMA kabla na wakati wa safari, kuzingatia maelekezo ya usalama na kuhakikisha maisha na mali zinalindwa wakati wa msimu wa mvua za Vuli 2026.

Hakuna maoni: