NAIBU Waziri wa Uchukuzi, Mheshimiwa David Kihenzile, ameipongeza Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kwa kuendelea kutoa utabiri wa hali ya hewa wenye usahihi wa zaidi ya asilimia 80, hatua inayosaidia Serikali na wananchi kuchukua tahadhari mapema dhidi ya athari za majanga ya asili.
Naibu Waziri Kihenzile ametoa pongezi 11 Septemba 2026 jijini Dar es Salaam wakati alipokutana na Mkurugenzi Mkuu wa TMA pamoja na wataalam wake na kupokea taarifa kuhusu mwenendo wa hali ya hewa nchini, ikiwemo matarajio ya mvua za El Nino na hatua zinazochukuliwa kuhakikisha taarifa za utabiri zinawafikia wananchi kwa wakati.
Naibu Waziri Kihenzile ameongeza kuwa usahihi wa taarifa za hali ya hewa una mchango mkubwa katika sekta mbalimbali za uchumi, hususan uchukuzi, kwa kuwa husaidia kupanga shughuli na kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza kutokana na mvua kubwa, mafuriko na upepo mkali.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TMA Dkt. Ladislaus Benedict Chang'a amesema mamlaka hiyo inaendelea kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji na utabiri wa hali ya hewa ili kuhakikisha taarifa sahihi zinapatikana na kuwafikia wadau kwa wakati.
Mkurugenzi Dkt. Chang'a ameongeza kuwa hatua hiyo inalenga kuongeza uwezo wa nchi kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na majanga yanayohusiana na hali ya hewa, ikiwemo mvua za El Nino zinazotarajiwa katika baadhi ya maeneo nchini.







Hakuna maoni:
Chapisha Maoni