Mkurugenzi wa Idara ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe Ofisi ya Waziri Mkuu - TAMISEMI Dkt. Rashid Mfaume amewataka wataalamu wa afya kutotegemea afua moja pekee katika kukabiliana na magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele NTDs, bali kuchambua kwa kina visababishi na mazingira yanayochangia kuendelea kwa magonjwa hayo katika jamii.
Dkt. Mfaume ameyasema hayo leo Septemba 12, 2026, jijini Arusha wakati akifungua kikao kazi cha Kuwajengea uwezo Waganga Wakuu wa Mikoa, Wilaya na Waratibu Magonjwa ya NTDs matumizi ya Scorecard pamoja na kufanya Tathimini ya Magonjwa ya Hayo.
Amesema ni muhimu kuangalia uhusiano kati ya kisababishi cha ugonjwa, binadamu na mazingira, ikiwemo upatikanaji wa maji na huduma za WASH, uelewa wa jamii, imani na tabia zinazoweza kuchangia kuenea kwa magonjwa hayo.
Aidha, Dkt. Mfaume amesisitiza umuhimu wa kutumia takwimu sahihi katika kufanya maamuzi, akieleza kuwa lengo la ukusanyaji wa takwimu lisiwe kutafuta nafasi nzuri katika scorecard, bali kuonesha hali halisi na kusaidia kubaini maeneo yenye changamoto.
“Pale ambapo scorecard inaonesha Halmashauri au Mkoa haujafanya vizuri, ni muhimu kuchambua sababu zilizo nyuma ya matokeo hayo na kuweka mipango madhubuti ya kukabiliana nazo, badala ya kutumia alama hizo kwa ajili ya kushindana au kujenga taswira pekee,” amesema Dkt. Mfaume
Pia amewataka viongozi kuhakikisha afua za NTDs zinaunganishwa kikamilifu katika mipango na bajeti za Halmashauri, pamoja na shughuli za kawaida za usimamizi wa huduma za afya, ikiwemo usimamizi shirikishi, tathmini ya ubora na mafunzo ili kuimarisha utendaji na ubora wa huduma.
“Rasilimali zilizopo zinapaswa kutumika kwa pamoja ili kuongeza ufanisi, kwa mfano: kuunganisha shughuli za usimamizi wa NTD na programu nyingine badala ya kila programu kuendesha shughuli zake kwa kujitegemea,” amesema Dkt. Mfaume

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni