Breaking

Jumanne, 8 Julai 2025

DIRA 2050 KUANZA KUTUMIKA JULAI MOSI MWAKA 2026-PROF MKUMBO.

 


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dokta Samia Suluhu Hassan, Julai 17 mwaka huu, anatarajiwa kuzindua Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 baada ya kukamilika katika hatua 12.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, amesema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na Jukwaa la Wahariri Tanzania, huku akisisitiza kuwa uzinduzi huo utafanyika jijini Dodoma. 

Waziri Profesa Kitila, amesema maandalizi yote ya dira hiyo yamekamilika ikiwemo kupitishwa na Baraza la Mawaziri, kisha Bunge kuipokea na kuiidhinisha kwa kuiwekea ulinzi.

Aidha, wakati wa ukusanyaji wa maoni, serikali imesema imeshirikisha makundi mbalimbali wakiwemo wanasiasa, na viongozi wastaafu zaidi ya 44, huku ikisisitiza kuwa maoni ya wananchi katika Dira 2050 itakayoanza kufanya kazi Julai Mosi mwaka 2026, yamezingatiwa.

Rais Dokta Samia, atakuwa ni Rais wa pili kuzindua Dira 2050 baada ya dira ya kwanza ya mwaka 2000 inayomalizikia mwaka huu 2025 kuzinduliwa na Rais Mstaafu Hayati Benjamin Mkapa.

Naye, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri nchini Tanzania, Deodatus Balile, amesisitiza umuhimu wa vyama vya siasa 19 vitakavyoshiriki Uchaguzi Mkuu mwaka huu kuwa na Ilani za Uchaguzi zenye kuakisi malengo na mipango iliyopo kwenye Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025/2050 ili kuwa na mtazamo wa pamoja wa Tanzania tuitakayo kufikia mwaka 2050.

Hakuna maoni: