Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Hassan Saidy amesema Wakala umejizatiti kuhakikisha 80% ya Watanzania wanatumia Nishati Safi ya Kupikia ifikapo mwaka 2034 kama ilivyoelekezwa katika Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia.
Amebainisha hayo Jijini Dar es Salaam, huku akisema mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia, umeelekeza ifikapo mwaka 2034; angalau 80% ya Watanzania wawe wanatumia nishati safi ya kupikia na REA ni miongoni mwa taasisi zilizopewa jukumu la kuhakikisha lengo hilo linafikiwa.
Alibainisha kuwa kwa sasa takriban asilimia 96 ya wananchi maeneo ya vijijini wanatumia kuni na mkaa kupikia na kwamba jukumu lililopo ni kuhakikisha wananchi hao wanaachana na matumizi ya nishati zisizo salama na kuanza kutumia nishati safi na salama.
Alitaja hatua mbalimbali zinazoendelea kuchukuliwa na REA ikiwemo uhamasishaji na uelimishaji wananchi kufahamu athari za kutumia nishati isio salama pamoja na kuwafahamisha faida za kutumia nishati safi ya kupikia, kuwarahisishia wananchi upatikanaji wa bidhaa za nishati safi jirani na maeneo yao na kuwezesha teknolojia za nishati yenyewe.
Aliongeza kuwa watu wengi hawaangalii gharama nyingine kama muda wanaotumia kusaka kuni na madhila mengine wanayokutana nayo huko porini wakati wakisaka kuni.
Alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuiwezesha REA kutekeleza jukumu la kusimamia upatikanaji wa nishati safi ya kupikia hasa ikizingitiwa kuwa yeye ni kinara wa nishati safi ya kupikia.
Alibainisha baadhi ya mafanikio ambayo yamepatikana tangu kuanza kutekeleza mkakati huo wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia ambayo ni pamoja na kuwezesha wananchi maeneo mbalimbali vijijini kuhama kupitia ruzuku iliyotolewa ya asilimia 50 kwenye majiko ya gesi ya kilo 6 na vichomeo vyake.
“Serikali inayoongozwa na Mhe. Rais Samia ilitoa ruzuku ya 50% kwenye mitungi ya gesi ya kupikia ipatayo 452,000 ambayo imeshaanza kusambazwa kwenye mikoa yote Tanzania Bara na zoezi linaendelea; sambamba na mitungi 110,000 ambayo ilisambazwa mwaka juzi kupitia Wabunge kwenye majimbo yao,” alisema Mhandisi Saidy.
Mhandisi Saidy vilevile alibainisha mradi wa mikopo nafuu wa kuwezesha ujenzi na uendeshaji wa vituo vya mafuta ya petroli na dizeli ulioanzishwa na REA ambao umelenga kuwasogezea wananchi wa vijijini huduma kwa gharama nafuu na ubora unaokubalika.


Hakuna maoni:
Chapisha Maoni