Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Mhe. Nurdin Babu ametoa wito kwa wakazi wa mkoa wa Kilimanjaro na maeneo ya jirani kujitokeza kwa wingi katika kambi ya huduma za uchunguzi na matibabu ya ubingwa na ubingwa bobezi bure yatakayotolewa na Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa kushirikiana na Vodacom Tanzania Foundation kuanzia Julai 25 hadi 27, 2025 katika viwanja vya Uhuru Park Manispaa ya Moshi.
Mhe. Babu ametoa wito huo alipokutana na baadhi wataalam watakaotoa huduma katika kambi hiyo kwa lengo la kujitambulisha na kueleza huduma watakazozitoa kwa kipindi chote watakachokuwa katika mkoa huo.
Mhe. Babu amebainisha kuwa wakazi wa mkoa huo na maeneo ya jirani wamekuwa na utamaduni wa kujitokeza kwa wingi pindi huduma kama hizo zinapotolewa na kuongeza kuwa ofisi yake itatoa ushirikiano wa kutosha ili kuhakikisha kuwa hawapati kikwazo chochote wakati wa kutoa huduma.
“Ninatoa rai kwa watu wote, kutumia fursa hii kuja kupata huduma za matibabu ya bure, serikali kupitia hospitali yetu ya Muhimbili kwa kushirikiana na wenzetu wa Vodacom Foundation wameamua kusogeza matibabu haya ya ubingwa bobezi bure karibu yenu, ni wajibu wa kila mmoja kunufaika na matibabu hayo” amesema Mhe.Babu
Huduma zitakazotolewa katika kambi hiyo ni pamoja na uchunguzi na matibabu ya macho, afya ya kinywa na meno, magonjwa ya akina mama na afya ya uzazi, magonjwa ya ngozi, magonjwa ya afya ya akili, sukari na homoni, matumizi sahihi ya dawa, vipimo vya maabara, saratani , tezi dume pamoja na elimu juu ya magonjwa yasiyoambukiza.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni