Katika kuadhimisha Siku ya Mazingira Duniani, Mkoa wa Dar es Salaam umefanya maadhimisho katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam, yakihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, wadau wa mazingira na wananchi. Maadhimisho hayo yalifanyika chini ya kaulimbiu ya “Dira 2050: Tuwajibike Kukijanisha Tanzania” yenye lengo la kuhamasisha jamii kushiriki kikamilifu katika uhifadhi wa mazingira na matumizi endelevu ya rasilimali za asili.
Akizungumza kwa niaba ya mgeni rasmi, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo amesema kila Mtanzania ana wajibu wa kushiriki katika juhudi za kuifanya Tanzania kuwa ya kijani kwa kupanda miti, kulinda vyanzo vya maji na kudhibiti uchafuzi wa mazingira. Amesema hatua hizo ni muhimu katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kuhakikisha maendeleo endelevu ya taifa sambamba na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Mpogolo pia amelipongeza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kuhamasisha na kusimamia shughuli za uhifadhi wa mazingira nchini. Aidha, amewasihi NEMC kuendelea kushirikiana kwa karibu na halmashauri mbalimbali ili kuimarisha usimamizi wa mazingira katika ngazi za serikali za mitaa na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa programu za uhifadhi wa mazingira.
Maadhimisho hayo yalihudhuriwa na taasisi mbalimbali zinazojihusisha na masuala ya mazingira ikiwemo NEMC, Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), pamoja na wadau kutoka sekta za umma na binafsi. Katika hafla hiyo, tuzo mbalimbali zilitolewa kwa taasisi, makundi na wadau waliofanya vizuri katika shughuli za uhifadhi na utunzaji wa mazingira, ikiwa ni sehemu ya kutambua mchango wao katika kulinda mazingira na kuhamasisha ushiriki mkubwa zaidi wa jamii katika kuifanya Tanzania kuwa safi, ya kijani na endelevu kwa vizazi vya sasa na vijavyo.




Hakuna maoni:
Chapisha Maoni