Baada ya sakata la mahojiano na kipindi cha Gen Talk cha Mjini FM, msanii wa Singeli Dogo Patten ametoa salamu za shukrani kwa wote waliomsimamia katika kipindi cha mjadala mkali mitandaoni.
Kupitia ujumbe wake, Patten ameandika:
“Asante sana kwa kila mmoja aliyesimama nami wakati wa changamoto hii. Nimejifunza mengi, na moyo wangu umejawa na shukrani kwa upendo na uungwaji mkono mkubwa kutoka kwa mashabiki wangu, watu maarufu, waandishi wa habari, na Watanzania wema.”
Ameishukuru Wizara ya Sanaa kupitia Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari na BASATA kwa kuchukua hatua za kulinda maadili ya tasnia na kuthibitisha kuwa utu na heshima bado vina nafasi kubwa katika jamii.
Patten amesisitiza kuwa sakata hili halijamvunja moyo bali limemjenga zaidi:
“Msiache kunipa imani, niendelee kuwalipa uwezo,” aliandika akimshukuru pia timu yake, DJ Boba.
Kauli hii inakuja baada ya watangazaji wa Gen Talk kufungiwa na kupigwa marufuku kujihusisha na kazi za habari kutokana na kosa la kumlazimisha msanii kutoa taarifa binafsi na kumtweza hewani, huku wakiwa hawana sifa za utangazaji.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni