Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo tarehe 31 Julai 2025, ameweka jiwe la msingi katika Kongani ya Viwanda ya Kwala (Kwala Industrial Park), iliyopo eneo la Kwala, Kibaha Vijijini mkoani Pwani.
Katika tukio hilo la kihistoria, Mhe. Rais aliongoza sherehe rasmi kwa kuvuta kitambaa kuashiria uwekaji wa jiwe la msingi, kama ishara ya kuanza kwa safari ya mageuzi makubwa ya viwanda nchini.
Kongani ya Kwala inalenga kuwa kitovu kikubwa cha viwanda nchini, kwa malengo ya kujenga viwanda 2000, huku kwa sasa ikiwa tayari na viwanda 12 vinavyoendelea kujengwa na kuanza uzalishaji, ndani ya eneo lenye ukubwa wa ekari 2,500.
Katika hotuba yake, Mhe. Rais Samia alisisitiza umuhimu wa kongani hiyo katika kufanikisha ajenda ya uchumi wa viwanda, kuongeza ajira, kukuza uchumi wa mkoa wa Pwani na taifa kwa ujumla.
Kongani ya Kwala inatarajiwa kuwa mfano wa mafanikio ya uwekezaji wa ndani na nje, ikichangia kwa kiasi kikubwa katika mpango wa kitaifa wa maendeleo ya viwanda unaolenga Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati unaotegemea uzalishaji ifikapo mwaka 2030.
📸 Tazama picha za tukio hili kupitia kurasa rasmi za Madelemo News.
📍 #KwalaIndustrialPark #SamiaSuluhu #MadelemoNews



Hakuna maoni:
Chapisha Maoni