Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), Dkt. Stella Bitanyi, leo Julai 18, 2025 amekuwa mgeni rasmi katika mechi ya kirafiki ya mchezo wa mpira wa miguu iliyowakutanisha watumishi kutoka idara mbalimbali zilizo chini yake.
Mchezo huo uliopigwa saa 10 jioni katika uwanja wa Mifugo Complex Arena, Veterinari – Temeke, uliwashindanisha Muunganiko wa TVI na CIDB dhidi ya Muunganiko wa TVLA Makao Makuu na CVL, ambapo timu ya TVLA-HQ/CVL iliibuka kidedea kwa ushindi wa magoli 4-2.
Akizungumza mara baada ya mchezo huo, Dkt. Bitanyi aliwapongeza wachezaji wote kwa ushiriki wao na kuonesha mshikamano kupitia michezo, huku akisema kuwa michezo ni sehemu muhimu ya afya ya mwili na akili, hasa katika mapambano dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza.
"Moja ya majukumu ya TVLA ni kupambana na magonjwa yasiyoambukiza kwa watumishi, na kwa kuwa michezo ni njia muhimu ya kuzuia magonjwa hayo, nawahakikishia kuwa nitayapa kipaumbele masuala ya michezo katika mwaka huu wa fedha.”
“TVLA sasa ina timu nzuri ya mchezo wa mpira wa miguu. Tumejipanga kushiriki kikamilifu mashindano ya SHIMIWI na SHIMUTA mwaka huu. Nitahakikisha michezo inapewa kipaumbele ndani ya mwaka huu wa fedha"alisema Dkt. Bitanyi.
Katika kuthamini jitihada za wachezaji, Dkt. Bitanyi alitoa zawadi ya Shilingi milioni mbili kwa timu iliyoshinda na shilingi laki nane kwa timu iliyopoteza mchezo, kama motisha na kuhamasisha ushiriki zaidi wa michezo kazini.
Akizungumza kwa niaba ya wachezaji wenzake, Dkt.Fred Makoka alimhakikishia Mtendaji Mkuu kuwa wataendelea kuhamasishana kufanya mazoezi,
“Michezo ni afya na pia huleta furaha. Tutaendelea kushirikiana kuhakikisha kila mfanyakazi anashiriki.” Alisema Dkt. Makoka
Kwa upande wa washindi, magoli manne yalifungwa na Dkt. Emmanuel Ngassa – goli la kwanza, Juma Malisa – goli la pili, Godfrey Minga – goli la tatu na Jafari Mkamba – goli la nne. Mchezo huo ulishuhudia pasi mbili za mabao (assist) kutoka kwa Fihiri Mbawala, na moja kutoka kwa Sailen.
Kwa upande wa Muunganiko wa TVI na CIDB, goli lao la kwanza lilifungwa na Said Macha, huku goli la pili likiwa la kujifunga, lililofungwa na Dkt. Ngassa wa TVLA-HQ.
Kwa mujibu wa waandaaji, mchezo wa marudiano unatarajiwa kuchezwa Ijumaa ya Julai 25, 2025, katika uwanja wa Kibaha, mkoani Pwani, kuanzia saa 10 jioni.





Hakuna maoni:
Chapisha Maoni