Breaking

Jumatano, 9 Julai 2025

WATAALAM TANCDA WAONYA MADHARA YATOKANAYO NA BISKUTI ZA SUKARI.



Wakati leo ikiwa ni Siku ya Kimataifa ya Biskuti zenye Sukari, wataalamu wa masuala ya lishe kupitia Shirikisho la Magonjwa Yasiyoambukiza-TANCDA, wameonya kuhusu madhara yatokanayo na Bisikuti hizo.

Ripoti ya TANCDA ya mwaka 2023 inaonesha kuwa asilimia 11 ya Watanzania wana ugonjwa wa kisukari, na wengi hawajui hali yao, huku ulaji wa sukari kupita kiasi ukiwa ni miongoni mwa visababishi.

Licha ya ladha yake kuvutia na kupendwa na watu wa rika zote, hasa watoto, wataalamu wa afya wameendelea kutoa tahadhari kuhusu matumizi ya kupita kiasi ya vyakula vyenye sukari ambavyo vinaweza kusababisha madhara makubwa kwa afya.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani-WHO, matumizi ya sukari yaliyopitiliza yanapaswa kuwa chini ya asilimia 10.

Aidha, uzito kupita kiasi na unene, tafiti zinaonyesha kuwa zaidi ya asilimia 27 ya watu wazima hapa nchini wana uzito mkubwa au ni wanene, hali inayochochewa na ulaji wa sukari nyingi bila mazoezi.

Lakini je, wananchi wanaelewa madhara hayo? hawa hapa baadhi yao wakieleza mitazamo yao kuhusu ulaji wa biskuti zenye sukari na matumizi ya sukari kwa ujumla.

Akizungumza na Uhuru FM, Afisa Lishe kutoka Shirikisho la Magonjwa Yasiyoambukizwa Tanzania-TANCDA, Adelina Munuo, ameitaka jamii kuwa makini na kiwango cha sukari kinachotumika kwenye bidhaa kwa kuwa ulaji wa sukari kupita kiasi unachangia ongezeko la magonjwa sugu yasiyoambukizwa.

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya, asilimia 40 ya watoto wa shule nchini wanakabiliwa na matatizo ya kuoza meno kutokana na ulaji wa mara kwa mara wa vyakula vyenye sukari, ikiwemo Biskuti.

Taarifa ni kwamba, Siku ya Kitaifa ya Biskuti za Sukari huadhimishwa ikiwa ni miongoni mwa sikukuu tamu na za kufurahisha zaidi kwa wapenzi wa vitafunwa, ni siku rasmi ya kuruhusu tamaa ya sukari kushinda.



Biskuti hizi zimekuwa maarufu katika nyumba nyingi, si tu nchini Marekani bali pia duniani kote, ingawa zinaonekana kuwa rahisi, biskuti za sukari hutumika kwenye matukio mbalimbali kama Valentine’s Day, Pasaka, Krismasi, na siku za kuzaliwa.

Hakuna maoni: