Breaking


Alhamisi, 7 Agosti 2025

𝑻𝑭𝑺 𝒀𝑨𝑻𝑨𝑵𝑮𝑨𝒁𝑨 𝑭𝑼𝑹𝑺𝑨 𝒁𝑨 𝑼𝑾𝑬𝑲𝑬𝒁𝑨𝑱𝑰 𝑾𝑨 𝑴𝑰𝑺𝑰𝑻𝑼 𝑵𝑨𝑵𝑬𝑵𝑨𝑵𝑬

Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) umetumia jukwaa la Maonesho ya Nanenane yanayoendelea katika Viwanja vya Nzuguni, jijini Dodoma, kutangaza fursa lukuki za uwekezaji zinazopatikana katika sekta ya misitu na nyuki.

Maonesho hayo, yanayofanyika kuanzia Agosti 1 hadi 8, 2025, yamekuwa fursa muhimu kwa TFS kuelimisha wananchi na wawekezaji kuhusu maeneo yenye utajiri wa rasilimali zinazoweza kuongeza kipato cha mtu mmoja mmoja na pato la Taifa kwa ujumla.

Akizungumza katika Kongamano la Uwekezaji wa Kanda ya Kati lililofanyika ndani ya maonesho hayo Agosti 6, 2025, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi, Gilead Teri, aliyemwakilisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, alisema serikali imeendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini ili kuvutia wawekezaji wa ndani na nje.

“Tunaendelea kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji, ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa mikopo yenye riba nafuu, ili kuongeza thamani ya mazao yanayozalishwa nchini,” alisema Teri.

Kwa upande wake, Mhifadhi Mkuu Husna Msagati kutoka TFS aliyemwakilisha Kamanda wa Kanda ya Kati, Mathew R. Kiondo alieleza kuwa wakala huo umekasimiwa kusimamia rasilimali za misitu na nyuki nchini kwa kuhakikisha matumizi yake ni endelevu kwa kizazi cha sasa na kijacho.

Alibainisha kuwa Kanda ya Kati inayojumuisha mikoa ya Dodoma, Singida na Manyara ina jumla ya hifadhi 47, sawa na asilimia 10 ya hifadhi zote za Tanzania Bara. Hifadhi hizo zinajumuisha hifadhi za mazingira asilia (3), hifadhi za nyuki (4), vichaka vya Itigi (20) na misitu ya kawaida (21).

“Misitu hii ina fursa nyingi za kiuchumi ambazo wananchi na wadau mbalimbali wanaweza kuzitumia kuongeza kipato kupitia shughuli za utalii ikolojia, utalii wa nyuki, uwekezaji kwenye malazi ya wageni, bustani za wanyamapori na maeneo ya camping,” alisema.

Aidha, Msagati alisisitiza kuwa TFS imefungua milango kwa wawekezaji kuanzisha viwanda vya kuchakata mazao ya nyuki, ili kuongeza thamani ya bidhaa hizo na kuimarisha masoko ya ndani na nje ya nchi.

Baadhi ya maeneo yaliyotajwa kuwa na fursa za uwekezaji katika Kanda ya Kati ni pamoja na Hifadhi za Chenene, Nou, Vichaka vya Itigi, Michoro ya Miambani Kolo (Kondoa), Chiyami, Bereko, Hasama, Mlima Hanang, Haraa, na Kilima Tinde (viewpoint ya Bonde la Ufa na njia ya watumwa). Pia ipo fursa ya kilimo cha migundi katika eneo la Wembere.

Hakuna maoni: