Mkuu wa Wilaya ya Iramba, mkoani Singida, Mhe. Suleiman Mwenda amewahimiza Watanzania kuthamini na kuamini tiba asilia zinazotokana na rasilimali za misitu, akisema zimekuwa msaada mkubwa wa kiafya katika jamii nyingi duniani.
Akizungumza mara baada ya kupata huduma ya kudungwa na nyuki (api-therapy) Agosti 05, 2025 kwenye banda la Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), katika Maonesho ya Nanenane yanayoendelea kwenye Viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma, Mkuu huyo wa Wilaya alisema.
“Huduma kama hizi ni uthibitisho kuwa rasilimali zetu za misitu si tu ulinzi wa mazingira, bali pia chanzo cha afya njema. Ni jambo la kujivunia kuona taasisi kama TFS wakifanya kazi hii kwa weledi na kujitolea kwa jamii.”
Huduma hiyo inayotolewa bure kwa wananchi ni sehemu ya juhudi za TFS kuelimisha umma kuhusu manufaa ya uhifadhi wa mazingira kupitia tiba asilia. Kwa mujibu wa Mhifadhi Brenda Mwakipesile kutoka Hifadhi ya Mazingira Asilia ya Vikindu, tiba hiyo husaidia kuimarisha kinga ya mwili, kupunguza maumivu ya viungo, kuboresha mzunguko wa damu, na kusaidia afya ya akili.
“Tumeileta huduma hii bure kwa wananchi ili kuwaonesha kuwa uhifadhi wa misitu hauishii kwenye miti pekee, bali unaweza pia kuzaa tiba salama, asilia na zenye manufaa ya kiafya,” alisema Mhifadhi Brenda.
Maonesho ya Nanenane kitaifa yanaendelea hadi Agosti 8, 2025.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni