Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) imeendelea kuchochea ukuaji wa biashara za kimataifa baada ya kupokea ujumbe maalum kutoka nchini Belarus kwa lengo la kujadili fursa za ushirikiano wa kibiashara na uwekezaji kati ya mataifa haya mawili.
Mazungumzo hayo yaliyofanyika Makao Makuu ya TanTrade jijini Dar es Salaam yalilenga kuimarisha mahusiano ya kiuchumi, kubadilishana uzoefu na kufungua milango ya biashara katika sekta mbalimbali zenye mchango mkubwa kwa maendeleo ya taifa.
Akizungumza kuhusu fursa zilizopo nchini Tanzania, Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade, Dkt. Latifa M. Khamis, alibainisha kuwa Tanzania ina nafasi kubwa za uwekezaji na biashara katika sekta muhimu zikiwemo madini, kilimo, afya, usafirishaji na burudani. Alieleza kuwa sekta hizo zinaendelea kukua na kutoa fursa kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa National Export Promotion Centre ya Belarus, Mikalai Barysevich, alieleza kuwa Belarus imeendelea kufanya maendeleo makubwa katika teknolojia za viwandani, jambo linaloweza kuleta manufaa makubwa kwa Tanzania kupitia ushirikiano wa kiteknolojia na uhamishaji wa ujuzi.
Aidha, TanTrade ilitumia kikao hicho kuwakaribisha Mikalai Barysevich pamoja na wadau wa biashara kutoka Belarus kushiriki katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam yatakayofanyika kuanzia Juni 28, 2026. Maonesho hayo yanatarajiwa kuwa jukwaa muhimu la kuonesha bidhaa, huduma na teknolojia mbalimbali kutoka mataifa tofauti duniani.
Ushirikiano huu unatarajiwa kuongeza mtandao wa biashara, kuimarisha uwekezaji na kuchochea ukuaji wa uchumi kati ya Tanzania na Belarus.



Hakuna maoni:
Chapisha Maoni