Breaking


Jumanne, 28 Aprili 2026

TANZANIA YANG’ARA SEKTA YA MADINI, YAPONGEZWA KIMATAIFA KWA KUCHOCHEA UCHUMI



Sekta ya madini nchini Tanzania imeendelea kujipatia sifa kimataifa baada ya kupongezwa kwa mchango wake mkubwa katika kukuza pato la taifa (GDP). Mafanikio haya yameifanya Tanzania kuwa mfano wa kuigwa na nchi kadhaa za Afrika Mashariki, zikiwemo Kenya, Somalia na Sudan Kusini, ambazo zimeonyesha nia ya kujifunza zaidi kuhusu usimamizi na maendeleo ya sekta hiyo.


Pongezi hizo zimetolewa wakati wa Mkutano wa Kimataifa wa Uwekezaji wa Madini (Kenya Mining Investment Conference and Expo – MICE 2026), unaofanyika jijini Nairobi kuanzia Aprili 28 hadi 29, 2026. Mkutano huo umezikutanisha pamoja viongozi wa serikali, wawekezaji na wadau wa sekta ya madini kutoka mataifa mbalimbali barani Afrika.

Akizungumza katika mdahalo wa mawaziri wa madini, Waziri wa Madini wa Tanzania, Mhe. Anthony Mavunde, alieleza kuwa mafanikio yaliyopatikana yametokana na uongozi thabiti wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Alisisitiza kuwa serikali imeendelea kuweka mazingira rafiki kwa uwekezaji, kuimarisha usimamizi wa rasilimali, na kuhimiza uongezaji thamani wa madini ndani ya nchi.

Kwa upande wake, Rais wa Kenya, Mhe. William Ruto, aliyetungua rasmi mkutano huo, alizitaka nchi za Afrika Mashariki kuimarisha ushirikiano katika sekta ya madini. Alibainisha kuwa kuongeza thamani ya rasilimali hizo kutasaidia kukuza uchumi wa ukanda huo na kuongeza ushindani katika soko la kimataifa.

Katika hatua nyingine, Waziri Mavunde aliwahimiza wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuchangamkia fursa zilizopo Tanzania. Alieleza kuwa nchi imejipanga vyema katika maeneo ya uchimbaji, uchenjuaji na uongezaji thamani wa madini, huku ikiendelea kuboresha sera na miundombinu inayorahisisha uwekezaji.


Nchi za Kenya, Somalia na Sudan Kusini zimetaja Tanzania kuwa chanzo muhimu cha uzoefu katika sekta ya madini, hasa katika mifumo ya usimamizi, uendelezaji wa wachimbaji wadogo na mikakati ya kuongeza thamani ya rasilimali.


Aidha, Waziri wa Madini wa Kenya, Hassan Ali Joho, alisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kikanda badala ya ushindani, akieleza kuwa kwa kufanya kazi pamoja, nchi za Afrika zinaweza kunufaika zaidi na rasilimali zake.


Naye Waziri wa Petroli na Rasilimali Madini wa Somalia, Dahir Shire Mohamed, alieleza kuwa nchi yake inaendelea kujifunza kutoka Tanzania ili kujenga mifumo imara ya usimamizi wa rasilimali.


Mawaziri wengine walioshiriki katika mjadala huo ni pamoja na Waziri wa Maendeleo ya Madini wa Nigeria, Oladele Henry Alake, na Waziri wa Madini wa Sudan Kusini, Losuba Ludoru Wongo.


Kwa ujumla, mjadala huo umeonyesha dhamira ya pamoja ya mataifa ya Afrika kuimarisha ushirikiano katika sekta ya madini, kwa lengo la kuongeza thamani, ajira na mapato yatokanayo na rasilimali za bara hili.

 

Hakuna maoni: