Breaking


Jumanne, 28 Aprili 2026

ONYO LA WAZIRI CHONGOLO KWA WAUZAJI WA MBEGU ZISIZO NA UBORA.

WIZARA ya Kilimo,katika Mwaka wa fedha wa 2026/2027,imejipanga kuimarisha uthibiti wa ubora wa mbegu kwak utoa mafunzo kwa vitendo 148 kwa wakulima na wauzaji wa mbegu ili kuwalinda dhidi ya hasara na kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao.


Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo,akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa Mwaka 2026/2027,Bungeni Jijini Dodoma,amesema mafunzo hayo yatalenga kuwawezesha wakulima kutambua tofauti kati ya mbegu bora na zisizo na ubora ili kuepuka hasara.


Amesema msingi wa mapinduzi ya kilimo unaanzia kwenye matumizi ya mbegu bora ambazo hubeba hatma ya mavuno, tija na usalama wa chakula nchini.


Amebainisha kuwa serikali imekuwa ikipokea malalamiko kutoka kwa baadhi ya wakulima kuhusu uwepo wa mbegu zisizo na ubora zinazouzwa na wafanyabiashara wasio waaminifu.


Kufuatia hali hiyo Waziri Chongolo ametoa onyo kali kwa wafanyabiashara wanaojihusisha na uuzaji wa mbegu zisizo na ubora, akisisitiza kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.


Pia amewataka wakulima kuwa makini kwa kununua mbegu kutoka kwa mawakala waliosajiliwa na kuhakikisha wanakagua nembo za uthibiti ubora kwenye vifungashio.


Katika kuimarisha zaidi mfumo wa uthibiti wa mbegu nchini, amesema Tanzania Official Seed Certification Institute itanunua mtambo wa kuchapisha lebo za uthibiti ubora zitakazotumika kwenye vifungashio vya mbegu, hatua itakayoongeza ufanisi na kupunguza vihatarishi vya kiusalama.

Hakuna maoni: