Breaking


Jumanne, 5 Agosti 2025

RAIS SAMIA AWAFUTA MACHOZI YA KUNI AKINAMAMA NCHINI


Rais Dokta Samia Suluhu Hassan ametoa ruzuku ya shilingi Bilioni-9.4 kwenye majiko banifu nchini, huku Kaya 200,000 zikinufaika.

Hii ni baada ya Wakala wa Nishati Vijijini-REA, kutekeleza mradi wa zaidi ya shilingi bilioni-9 wa kusambaza majiko yaliyoboreshwa maarufu majiko banifu 200,000 kwa bei ya ruzuku ya asilimia 80 hadi 85 kote nchini.

Hayo yamesemwa na mwakilishi wa REA Mkoa wa Morogoro, Mhandisi Cecilia Msangi, wakati akimtambulisha mtoa huduma aliyeshinda zabuni ya kusambaza majiko hayo Mkoani humo, Kampuni ya Burn Manufacturing Tanzania Ltd.

Amemshukuru Rais Dkt.Samia kwa kuwa kinara wa kampeni hiyo ya Nishati Safi ya Kupikia ambayo amesema kwa jitihada zake binafsi hatua zimechukuliwa hususan za kuwanusuru akina mama kutokana na madhara ya moshi wa kuni sambamba na uhifadhi wa mazingira.

Rais Dkt.Samia alitoa maelekezo mahususi ya kuhakikisha wananchi wanawezeshwa ili kuachana na matumizi ya kuni na mkaa kupikia ikiwa ni utekelezaji wa mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia ambao umeelekeza ifikapo Mwaka 2034, asilimia 80 ya wananchi wawe wanatumia nishati safi ya kupikia.

Akizungumza kuhusu utekelezaji wa mradi kwa Mkoa wa Morogoro, Msangi amesema majiko banifu 8,366 yatatolewa kwa bei ya ruzuku ya shilingi 14,694 kwa kila jiko.

Naye, Meneja wa Kampuni ya Burn Manufacturing Tanzania Ltd, John Mtui amesema kampuni hiyo imeshinda zabuni ya kusambaza majiko banifu 39,286 katika Mikoa ya Morogoro, Ruvuma, Kagera na Tabora ambayo ni sawa na zaidi ya shilingi bilioni-2.

Hakuna maoni: