Serikali kupita Ofisi ya Msajili wa Hazina, na Kampuni ya Perseus Mining Limited, zimesaini mkataba wa nyongeza wa umiliki wa hisa katika mradi wa Dhahabu wa Nyanzaga, hatua inayochukuliwa kuwa ni kiungo muhimu cha ukuaji wa uchumi na ustawi wa wananchi.
Mkataba huo uliosainiwa katika hafla iliyofanyika Wilayani Sengerema, mkoani Mwanza, unaongeza umiliki wa Serikali, kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina kutoka asilimia 16 hadi 20 katika Kampuni ya Ubia ya Sotta Mining Corporation Limited, ambayo inasimamia utekelezaji wa mradi mkubwa wa dhahabu unaotekelezwa kwa ushirikiano wa Perseus na Serikali.
Mkataba huo umesainiwa na Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Johari, kwa upande wa Tanzania, na Mkurugenzi wa Kampuni ya Perseus, Lee-Anne de Bruin, mbele ya Waziri wa Madini, Anthony Mavunde.
Katika hafla hiyo, Mchechu, amesema nyongeza ya hisa inaashiria dhamira ya Serikali ya kuhakikisha sekta ya madini inawanufaisha Watanzania kwa njia endelevu na ya uwajibikaji.
Kwa upande wake, Waziri wa Madini, Mavunde, aliyekuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo, ameeleza kuwa mkataba huo ni hatua muhimu ya kuimarisha ushirikiano wa Serikali na Kampuni binafsi katika sekta ya madini.
Zaidi ya shilingi Trilioni-1 zinatarajiwa kuwekezwa kwenye mradi huo na kwamba Serikali itaendelea kusimamia utekelezaji wake kwa karibu kuhakikisha wananchi wanapata fursa za ajira, ushiriki wa wananchi kupitia huduma na bidhaa, na mapato makubwa kupitia kodi na gawio la hisa.
Naye, Mkurugenzi wa Kampuni ya Perseus, Lee-Anne de Bruin, ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kufanikisha mazungumzo na kusaini mkataba huo wa nyongeza unaowezesha kuanza uzalishaji mwanzoni mwa mwaka 2027.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni