Breaking


Jumatatu, 4 Agosti 2025

TANESCO YAZINDUA MFUMO WA KUPOKEA TAARIFA ZA SIRI KWA WANANCHI

 

Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limezindua rasmi mfumo mpya wa kupokea taarifa za siri ujulikanao kama Whistleblower Portal ambao unalenga kurahisisha upokeaji wa taarifa muhimu kutoka kwa wananchi kuhusu vitendo vinavyoathiri utoaji wa huduma bora za umeme nchini.

Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano na Huduma kwa Wateja wa TANESCO, Bi. Irene Gowele, amesema kuwa kwa kipindi kirefu shirika limekuwa likikumbwa na changamoto mbalimbali zinazokwamisha utoaji wa huduma endelevu, ikiwemo wizi wa umeme, uharibifu wa miundombinu na vitendo vya rushwa vinavyofanywa na baadhi ya watumishi.

“Uzinduzi wa mfumo huu ni hatua kubwa ya kimageuzi katika utendaji kazi wa TANESCO. Mfumo huu utasaidia kudhibiti uhalifu, kuimarisha uwajibikaji, na kulinda taarifa dhidi ya vitisho, hivyo kuongeza uaminifu wa umma kwa shirika letu,” alieleza Bi. Gowele.

Ameongeza kuwa taarifa zotezitakazowasilishwa kupitia mfumo huu zitahifadhiwa kwa siri, na waotoa taarifa watapewa miongozo sahihi ya hatua zinazofuata. “Tutashirikiana kikamilifu kushughulikia taarifa zote zitakazowasilishwa kupitia mfumo huu wa siri,”.


Kwa upande mwingine, TANESCO imewataka wananchi kote nchini kushiriki kikamilifu katika kutumia mfumo huu ili kusaidia kulinda rasilimali za shirika pamoja na maslahi ya Taifa kwa ujumla.


Wananchi wanaweza kutoa taarifa kwa kutumia njia mbili kuu:

1. Kupitia tovuti rasmi ya TANESCO: www.tanesco.co.tz kwa kubonyeza kiungo cha Whistleblower Portal na kujaza fomu salama ya taarifa.

2. Kupiga simu ya bila malipo kwa namba 180, kisha kuchagua namba 2 kuwasiliana na watoa huduma wa shirika.


Aidha, TANESCO inaendelea na kampeni yake ya kitaifa ya “Lipa Deni, Tukuhudumie”, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha huduma za umeme zinatolewa kwa ufanisi na kwa wakati katika maeneo yote ya nchi.


Hakuna maoni: