Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Mobhare Matinyi, amekutana na kufanya mazungumzo rasmi na Waziri wa Mambo ya Nje wa Sweden, Maria Malmer Stenergard, katika ofisi za Wizara ya Mambo ya Nje jijini Stockholm, kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia na kiuchumi kati ya Tanzania na Sweden.
Katika mazungumzo hayo Balozi Matinyi aliwasilisha salamu za dhati kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt. Samia Suluhu Hassan, akisisitiza dhamira ya Tanzania kuendeleza na kuimarisha mahusiano ya muda mrefu kati ya nchi hizo mbili, hasa katika maeneo ya biashara, uwekezaji, na maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Aidha, Balozi Matinyi alifichua kuwa hadi sasa, jumla ya kampuni 101 kutoka Sweden zimewekeza nchini Tanzania, kwa thamani ya jumla ya dola za Marekani milioni 313.04 na kutoa ajira takribani 3,877. Alieleza kuwa Tanzania inaendelea kuhamasisha zaidi wawekezaji wa Kiswidi kushirikiana na sekta binafsi na ya umma nchini katika kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Sweden, Stenergard, alieleza kuwa Sweden ina nia thabiti ya kuendeleza ushirikiano wake na Tanzania, hususan katika nyanja za biashara na uwekezaji. Pia alitambua mchango wa Tanzania katika kudumisha amani na usalama wa kimataifa, na kupongeza msimamo wake katika kusaidia kutafuta suluhu ya kudumu ya mgogoro kati ya Ukraine na Urusi.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni