Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania-TPA imechukua hatua ikiwemo uboreshaji wa Miundombinu, kusimika mifumo bora ya TEHAMA na kushirikisha wadau wa sekta binafsi wakiwemo waendeshaji wa Bandari, ili kuongeza ufanisi katika kuhudumia Shehena za ndani na nje ya nchi kupitia katika bandari za Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Plasduce Mbossa wakati akifungua kikao cha Wadau wa Usafirishaji wa Shehena kupitia Ushoroba wa kati, kilichofanyika Bagamoyo, Naibu Mkurugenzi Mkuu, Dokta Baraka Mdima, amesema, hatua hizo zilichukuliwa na zinaendelea kuchukuliwa na TPA kwa lengo la kuongeza ufanisi na kuboresha tija Bandarini, ziende sambamba na kujenga utamaduni wa Uadilifu na Uwajibikaji kwa wafanyakazi wake, wateja na wadau ili kurahisisha ufanyaji biashara kupitia ushoroba wa kati.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Martin Masunga, amesema maoni yote yaliyotolewa na wadau yamepokelewa na yatafanyiwa kazi na Serikali ili kurahisisha ufanyaji wa Biashara na kuondoa ucheleweshaji kupitia Ushoroba wa kati.
Kikao hiki cha wadau wa Usafirishaji kimeandaliwa na TPA chini ya Usimamizi wa Wizara ya Uchukuzi na kimehudhuriwa na wadau wakiwemo Chama cha Mawakala wa Meli-TASAA, Chama cha Mawakala wa Forodha-TACAS, Baraza la Wasafirishaji-TSC, Wamiliki wa Bandari Kavu-CIDAT, Chama cha Wasafirishaji Tanzania-TAT, na Chama cha Wamiliki wa Malori madogo na ya kati-TAMSTOA.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni