Breaking


Ijumaa, 22 Agosti 2025

TRA KUWAWEZESHA WAFANYABIASHARA WASIO RASMI KUJISAJILI

 

Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Yusuph Juma Mwenda amesema kuwa TRA imeanza jitihada za kuwawezesha wafanyabiashara kwa kufungua madawati ya huduma mikoa yote na wilaya zote ili kuwarahisishia kujisajili kwa urahisi. 

Kamishna Mwenda ameyasema hayo leo tarehe 22.08.2025 katika mkutano wa  Wakurugenzi Watendaji wa makampuni mbalimbali Tanzania ulioandaliwa kwa ushirikiano wa Shirikisho la Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) na TRA uliofanyika jijini Dar es Salaam. 

Bw. Mwenda amesema moja ya  lengo la kuanzisha Madawati ya Uwezeshaji biashara ni kuweza kusajili wafanyabiashara ambao hawajarasimishwa ili kuongeza wigo wa kodi na  kupunguza kodi. 

Amebainisha kuwa bado kuna kiwango kikubwa cha ukwepaji wa kodi nchini, ikilinganishwa na

mchango wa kodi katika pato la Taifa, ambacho ni chini ya asilimia 15, kiwango kilicho chini ikilinganishwa na nchi zilizopo chini ya Jangwa la Sahara.

Bw. Mwenda ameahidi TRA kuendelea kupambana na wanaokwepa kodi kwa kuwachukulia hatua za kisheria, akisisitiza kuwa TRA haiko kinyume na wafanyabiashara wa nje ila ipo kinyume na mfanyabiashara yeyote asiezingatia sheria za kodi. 

Aidha, Kamishna Mkuu Mwenda ameendelea  kuwakumbusha wafanyabiashara wa huduma za malazi mtandaoni (Airbnb) kujisajili kabla ya tarehe 01.09.2025 na wanaofanya biashara nyingine za mtandaoni kujisajili kabla ya tarehe 01.01.2026. 

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirikisho la Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) Bw. Raphaely Maganga, amesema kuwa TRA inapaswa kuendelea na jitihada za kuwahamasisha wafanyabiashara wengi kulipa kodi kwa hiari ili kupunguza viwango vya  kodi.

Mkutano huu ulioandaliwa kwa ushirikiano wa TRA na TPSF ni sehemu ya jitahada za makusudi zinazofanywa na Kamishna Mkuu wa TRA kukuza mahusiano mema na kuwasikiliza wafanyabiashara  wa kila sekta na wadau wengine wa kodi ili kuweza kutatua changamoto zao na kuwawezesha kulipa kodi kwa hiari.

Hakuna maoni: