Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Dk. Mohammed Said Mohammed ‘Dimwa’ amebainisha maeneo 10 ambayo yamepewa kipaumbele katika ilani ya uchaguzi ya mwaka 2025/2030 kwa upande wa Zanzibar.
Akizungumza leo katika uzinduzi wa kampeni za mgombea urais wa Zanzibar kupitia CCM, Dk. Hussein Ali Mwinyi, uliofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja, Mkoa wa Mjini Magharibi, Dk. Dimwa alisema ilani hiyo imejikita katika kuimarisha umoja, mshikamano na amani ya wananchi.
“CCM inafanya hivyo kwa kuwa ina dhamana kubwa ya kuhakikisha hali ya amani na utulivu inaendelea kuimarika, sambamba na kujenga uchumi imara wenye usawa utakaonufaisha maeneo yote ya Zanzibar,” alisema Dk. Dimwa.
Aidha, alibainisha kuwa CCM imepanga kuzalisha ajira 350,000 kwa vijana katika sekta rasmi na zisizo rasmi, pamoja na kuongeza uzalishaji wa chakula ili kuimarisha uhakika wa upatikanaji wake.
Maeneo mengine yaliyoainishwa ni pamoja na kuimarisha mikopo kwa wajasiriamali, uanzishaji wa makazi bora ya miji, na kuhamasisha uwekezaji binafsi katika sekta za viwanda na kilimo.
Dk. Dimwa alisema serikali ya awamu ya nane tayari imetenga maeneo maalum ya uchumi na viwanda katika Dunga Zuze na Micheweni kwa ajili ya kuimarisha uchumi wa Zanzibar.



Hakuna maoni:
Chapisha Maoni