Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limeendesha msako maalum uliofanikisha kukamatwa kwa magari 15 yaliyokuwa yakiendeshwa bila namba rasmi za usajili. Msako huo umefanyika kuanzia Agosti 18 hadi 25, mwaka huu (2025).
Magari yaliyokamatwa kwa tuhuma za kutumia namba bandia za usajili jijini Dar es Salaam.
Magari ya Namba Bandia
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, amesema magari hayo yalikuwa yakitumia namba bandia aina ya SSH 2530, kinyume na Kifungu cha 13(1) cha Sheria ya Usalama Barabarani, Sura ya 168 ya mwaka 1973 (kama ilivyorekebishwa mwaka 2023).
Shehena ya Bangi Yabainika Kwenye Magunia ya Mchele
Katika oparesheni nyingine, Jeshi la Polisi lilimkamata Ramadhani Makala, mkazi wa Tabata, mnamo Agosti 11, 2025, kwa tuhuma za kusafirisha dawa za kulevya.
Mtuhumiwa huyo alikamatwa akitumia gari aina ya Fuso lenye namba za usajili T.733 AGT, akiwa na magunia 13 ya bangi yenye uzito wa kilo 239 yaliyokuwa yamefichwa kati ya magunia ya mchele, yakisafirishwa kutoka Morogoro kuelekea Dar es Salaam.
Sehemu ya shehena ya bangi iliyokamatwa na Jeshi la Polisi, ikiwa imechanganywa na magunia ya mchele.
Wizi wa Pikipiki
Vilevile, kati ya Agosti 12 hadi 20, 2025, polisi waliwakamata watuhumiwa wawili waliodaiwa kuhusika na wizi wa pikipiki. Watuhumiwa hao ni Hassan Hamis (mkazi wa Candle) na Elia Mapunda (mkazi wa Goba Njia Nne).
Kamanda Muliro amesema walikamatwa wakiwa na vipuli vya pikipiki pamoja na pikipiki sita zinazodhaniwa kuwa za wizi. Upelelezi unaendelea kubaini mtandao mzima wa uhalifu huo jijini Dar es Salaam.
Wito wa Ushirikiano
Jeshi la Polisi limesisitiza kuendelea na misako na doria za mara kwa mara kuhakikisha uhalifu unakomeshwa. Vilevile, Kamanda Muliro amewataka wananchi kushirikiana na vyombo vya usalama kwa kutoa taarifa mapema kuhusu uhalifu au viashiria vyake.
Madelemo News itaendelea kukuletea taarifa kuhusu operesheni na hatua zinazochukuliwa na Jeshi la Polisi kudhibiti uhalifu jijini Dar es Salaam.



Hakuna maoni:
Chapisha Maoni