Breaking


Jumapili, 7 Septemba 2025

TANESCO YAFANYA MATENGENEZO BILA KUZIMA UMEME KWA TEKNOLOJIA MPYA

Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limefanikiwa kufanya matengenezo kinga kwenye njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 220 kutoka Kituo cha Kupoza Umeme cha Chalinze hadi Kituo cha Kinyerezi jijini Dar es Salaam bila kuzima umeme, hatua inayojulikana kitaalamu kama live line maintenance.

Matengenezo hayo yalihusisha ubadilishaji wa vikombe vilivyoonekana kuwa na changamoto katika ukaguzi uliofanywa awali. Kwa kawaida, kazi hiyo ingeweza kulazimisha kuzimwa kwa umeme kwa muda mrefu, jambo ambalo lingewaathiri wateja wa maeneo mbalimbali.

Mhandisi kutoka Kitengo cha Usafirishaji Umeme, Philemon Tirukaizile, alisema teknolojia hiyo imeondoa kero ya kukatika kwa umeme wakati wa matengenezo.

“Bila teknolojia hii tungeweza kuzima njia ya kusafirisha umeme kwa zaidi ya masaa sita. Ina maana wateja kuanzia Chalinze, Mlandizi hadi Kibaha wangeweza kukosa huduma ya umeme,” alisema.

Kwa upande wake, msimamizi wa timu ya usafirishaji Mkoa wa Pwani, Sadiki Sadiki, alieleza kuwa zoezi hilo hufanyika kwa umakini mkubwa kwa kuzingatia usalama wa hali ya juu, na hufanywa na mafundi wabobezi waliopata mafunzo maalum.

“Kabla ya kazi, hufanyika mawasiliano na Kituo cha Kupoza Umeme ili kupata kibali. Kila fundi hutekeleza jukumu lake chini ya uongozi wa kiongozi wa timu anayetoa maelekezo ya nani afanye nini na wakati gani,” alisema.

Fundi mmoja aliyeshiriki katika zoezi hilo, Bahati Ramadhani, alisema ujuzi wa kutekeleza kazi za aina hiyo ameupata kupitia mafunzo maalum yaliyotolewa ndani ya shirika.

Teknolojia hii inalenga kupunguza upotevu wa umeme unaotokea wakati laini inapoachwa bila umeme, pamoja na kuondoa malalamiko ya wateja waliokuwa wakilazimika kukosa huduma kila kulipokuwa na matengenezo kinga.

Hakuna maoni: