Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Profesa Dos Santos Silayo, amesema mashirikiano ya kimkakati baina ya mataifa na wadau wa mazingira ndiyo tiba ya kudumu ya kuokoa misitu ya Miombo na kupunguza kasi ya uharibifu wa ardhi barani Afrika.
Akizungumza jana mbele ya mamia ya washiriki wa mkutano wa kimataifa wa nchi zinazotekeleza mradi wa usimamizi shirikishi wa misitu ya Miombo, Prof. Silayo alisema mataifa lazima yaweke makubaliano ya pamoja, ikiwemo mikataba ya huduma (service agreements) na hati za makubaliano (MoU), ili kuimarisha ushirikiano wa kikanda katika uhifadhi.
“Wadau wote wanaohusiana na shughuli zinazoweza kuharibu mazingira wanapaswa kushirikishwa na kuwa sehemu ya suluhisho. Ni kupitia mshikamano wa pamoja pekee ndipo tunaweza kuzuia uharibifu wa ardhi na misitu,” alisema Prof. Silayo.
Alibainisha kuwa Tanzania kupitia TFS tayari imetekeleza mikakati ya mfano ikiwemo kushirikiana na jamii na vikundi vya uhifadhi, kuwezesha mipango ya matumizi bora ya ardhi na kutoa hati za umiliki wa ardhi (CCROs) kwa wananchi, kuhamasisha kilimo endelevu, matumizi ya nishati safi ya kupikia, uhifadhi wa vyanzo vya maji na kuendeleza ufugaji nyuki pamoja na mnyororo wa thamani wa mazao yake.
Amesisitiza pia kuwa jamii lazima ziwezeshwe kupitia shughuli mbadala za kujipatia kipato, zipewe elimu ya mara kwa mara ya uhifadhi, na kuendeleza matumizi ya teknolojia za kisasa katika kufuatilia shughuli za misitu.
Katika hotuba yake, Prof. Silayo aliwashukuru wafadhili na waandaaji wa mkutano huo, akiwemo Mfuko wa Mazingira wa Dunia (GEF) kupitia OMR-Tanzania na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), akibainisha kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye sera, kanuni na mikakati wezeshi ya kuhifadhi misitu.
Baada ya uwasilishaji huo, Tanzania pia iliwasilisha mazao ya nyuki na nyenzo za uhifadhi zinazotumika katika mradi huo, hatua iliyothibitisha dhamira ya nchi kuendeleza nguvu ya pamoja katika kulinda na kuhifadhi misitu ya Miombo.





Hakuna maoni:
Chapisha Maoni