Sehemu ya 2: Kasri la Siri
Usiku uliofuata, Eliam hakuweza kulala. Kila alipozima taa, sauti ile nyororo ilimrudia kichwani:
“Usijaribu kufika hapa tena…”🤨🤨
Lakini moyo wa udadisi ulimshinda. Alijua kuna kitu kilichofichwa kwenye kasri lile. Alfajiri ilipofika, alichukua tochi, kombeo, na daftari lake dogo la kuchora. Safari hii, akaamua kuifuata njia ileile aliyomuona Amara akiipitia.
Ukungu ulikuwa mzito zaidi ya jana, na hewa ilibeba harufu ya maua yaliyooza na ardhi yenye unyevunyevu. Kadri alivyokaribia, alisikia mlio wa farasi ukigonga kokoto, kisha ukatulia. Kutoka mbali aliona mwanga hafifu ukimulika dirisha la kasri lililofunikwa na mizabibu — mlango wake mkuu ulikuwa umeandikwa kwa maandishi ya zamani:
“Siri ya damu haitakiwi kufichwa.”
Eliam alipiga moyo konde, akasukuma mlango ule. Ndani, vumbi lilimkaribisha kwa wingu zito, na paa lilikuwa na picha za familia ya kifahari wote wakiwa wamevaa mavazi meupe kama Amara, isipokuwa sura zao hazikuwa na macho, kana kwamba yalifutwa makusudi.
Ndipo akasikia sauti ya hatua nyuma yake. Polepole aligeuka.
Amara alisimama pale, akiwa amevalia gauni lile lile jeupe, lakini macho yake hayakuwa yale aliyoyaona shambani — yalikuwa meusi, yenye kina kisichoelezeka.
“Eliam…” alizungumza taratibu, “sasa umevuka mpaka ambao haupaswi kuvukwa.”
Kabla hajauliza chochote, taa zote ndani ya kasri zikazimika, na mlango uliojifunga kwa nguvu ukaacha sauti nzito ya chuma ikisikika…

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni