SEHEMU YA 3
Ndani ya giza la kasri, Eliam alihisi upepo mzito ukipita kando yake baridi iliyopenya mpaka kwenye mifupa. Akavuta pumzi kwa nguvu, akajaribu kuwasha tochi yake, lakini haikuwaka. Giza likawa limejaa sauti zisizoeleweka, zikimzunguka kutoka pande zote.
“Tulikuwa kama yeye… tulimwamini… tulilaaniwa,”
sauti moja ikanong’ona kwa uchungu.
Mara taa moja ya mshumaa ikawashwa peke yake. Mwangaza wake ukamuonyesha ukuta wenye maandiko ya damu kavu:
“Wale waliovunja kiapo cha damu, mioyo yao haitapumzika.”
Ndipo kivuli cha Amara kikatokea tena, safari hii kikiwa kando yake — lakini hakukuwa na farasi, wala tabasamu. Alimwangalia Eliam kwa huzuni.
“Sio wote walio ndani ya kasri hiki ni hai,” alisema kwa sauti ya chini.
“Wengine ni roho za familia yangu… waliofungwa hapa kwa kosa lililofanywa karne moja iliyopita.”
Eliam akasogea karibu, moyo ukipiga kwa nguvu.
“Na wewe… wewe ni nani hasa, Amara?”
Amara akanyamaza, machozi yakimtoka taratibu.
“Mimi ni miongoni mwao, Eliam. Nilipaswa kulala miaka mia moja iliyopita… lakini laana iliniacha hai nikiwa kati ya dunia mbili.”
Wakati Eliam akijaribu kuelewa maneno hayo, dirisha kubwa la kasri likafunguka kwa kishindo, upepo mkali ukapuliza mishumaa yote. Sauti nyingi zikaanza kulia kama upepo wa kaburi:
“Wakati wa damu unakaribia… mgeni lazima achague upande!”
Eliam akatazama Amara lakini alipogeuka tena, hakuwepo. Kitu pekee kilichobaki kilikuwa ni kofia yake ya majani na harufu hafifu ya maua yaliyokauka.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni