Breaking

Jumanne, 25 Novemba 2025

NEMC YATOA MWONGOZO KUDHIBITI KELELE NA MITETEMO

 

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limetoa taarifa kwa umma kuhusu hatua zinazochukuliwa kudhibiti kelele na mitetemo inayosababisha madhara kwa afya na mazingira nchini Tanzania.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Meneja wa Uzingatiaji wa Sheria wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira, NEMC, Hamadi Taimuru, amesema Serikali inaendelea kuchukua hatua madhubuti kwa kusimamia Sheria ya Usimamizi wa Mazingira, Sura ya 191, pamoja na kanuni zake.

Amesema sheria hiyo ndiyo msingi wa udhibiti wa kelele nchini, huku NEMC likiendelea kufuatilia viwango vya kelele, kutekeleza masharti ya kanuni, na kuhakikisha taasisi, biashara na wananchi wanazingatia matakwa ya mazingira.

Kwa mujibu wa Taimuru, Kanuni za Usimamizi wa Mazingira za mwaka 2015 zimeweka marufuku kwa mtu yeyote kutoa kelele kupita kiasi, na zimeainisha viwango maalumu kwa maeneo ya makazi, biashara, viwanda na taasisi nyeti kama hospitali na shule.

Aidha, amesema tafiti zinaonyesha madhara ya kiafya kutokana na kelele kupita kiasi, ikiwemo kupungua kwa usikivu, msongo wa mawazo, uchovu, shinikizo la damu, pamoja na matatizo ya usingizi. Kwa watoto, kelele zimeelezwa kupunguza umakini na kuathiri uwezo wa kujifunza.

Ameongeza kuwa NEMC inaendelea kufanya ukaguzi wa mara kwa mara, kutoa elimu kwa wananchi na maafisa wa mazingira, kuweka maeneo yasiyoruhusiwa kutoa kelele nyingi, na kupokea malalamiko kutoka kwa umma. Taasisi nyingine kama OSHA, Jeshi la Polisi, BASATA, Mamlaka za Serikali za Mitaa na jamii zinashirikiana kuhakikisha udhibiti wa kelele unatekelezwa kikamilifu.

NEMC imesisitiza kuwa ushirikiano wa taasisi zote na jamii, pamoja na kuelimisha umma na kufuatilia sheria kikamilifu, ni muhimu ili kuhakikisha afya na ustawi wa wananchi unalindwa na madhara yanayotokana na kelele na mitetemo yanapunguzwa.

Hakuna maoni: