Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wales Karia, alitembelea kambini kwa timu ya JKT Queens FC mjini Ismailia, nchini Misri, kwa lengo la kuwasalimia na kuwaongeza morali kuelekea mchezo wao wa mwisho wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Wanawake Afrika dhidi ya TP Mazembe ya DR Congo, utakaochezwa leo, 15 Novemba 2025, saa 12:00 jioni (Misri) sawa na saa 1:00 jioni (Tanzania), katika uwanja wa Suez Canal.
Katika picha ya pamoja na wachezaji, benchi la ufundi na viongozi wa timu, Rais Karia aliongozana na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFF), Dkt. Suleiman Jabir, wa nne kutoka kushoto waliokaa. Wengine waliokaa kwenye picha ni Azishi Kondo (Kocha Msaidizi), Shabani Dihile (Kocha wa Makipa), James Mhagama (Mkuu wa Msafara na Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Ruvuma), Meja Esta Ryoba (Mratibu wa JKT Queens FC), Ndugu Danny (Afisa wa TFF), Kessy Abdallah (Kocha Mkuu) na Frank Ndayeza (Daktari wa Timu).
JKT Queens FC, yenye alama mbili baada ya sare michezo miwili ya awali dhidi ya Gaborone United ya Botswana (0-0) na Asec Mimosas ya Ivory Coast (1-1), inahitaji ushindi wa magoli yoyote ili kufuzu hatua ya nusu fainali.
#Official-Isharoja✍🏾


Hakuna maoni:
Chapisha Maoni