Breaking

Jumatano, 26 Novemba 2025

WANARIADHA 155 KUSHIRIKI LADIES FIRST MSIMU WA SABA

 

Jumla ya wanariadha wanawake 155 wanatarajiwa kushiriki katika msimu wa saba wa mashindano ya riadha maarufu Ladies First yatakayofanyika kuanzia Novemba 29 hadi 30, 2025 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.


Mashindano hayo yanayoratibiwa kwa ushirikiano wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Japan (JICA) pamoja na Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), yatatanguliwa na semina ya wanariadha na waamuzi itakayofanyika Novemba 28, 2025 katika uwanja huo.


Akizungumza kuhusu maandalizi ya mashindano hayo leo Novemba 26, 2025 mbele ya wanahabari, Katibu Mtendaji wa BMT, Neema Msitha, alisema maandalizi yote yamekamilika na kwamba mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Prof. Palamagamba Kabudi. Msitha alisema lengo la mashindano hayo ni kuunga mkono jitihada za wanawake katika mchezo wa riadha, yakihusisha washiriki kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar.


Naye Rais wa RT, Rogath Stephen, alisema mashindano hayo yamekuwa na mchango mkubwa kwa taifa kutokana na kuongezeka kwa idadi ya wanariadha wa kike tofauti na miaka ya nyuma.


Kwa upande wake, mwanariadha mkongwe na muasisi wa Ladies First, Kanali Mstaafu Ikangaa, alisema wanariadha wengi waliowahi kufanya vizuri katika ngazi mbalimbali wamepitia mashindano hayo. Ameipongeza BMT kwa juhudi inazofanya katika kuibua na kukuza vipaji vya watoto wa kike.


#Official-Isharoja✍🏾✍🏾✍🏾

Hakuna maoni: