Breaking

Jumatano, 12 Novemba 2025

WANAJESHI WA MAREKANI WAWASILI CARIBBEAN

 

Kikosi cha wanamaji cha Marekani kilichojikita katika meli kubwa zaidi ya kivita duniani, USS Gerald R Ford, kimewasili katika visiwa vya Caribbean, Jeshi la Wanamaji la Marekani limethibitisha.

Kuwasili kwa wanajeshi hao ambako ni agizo la Rais Donald Trump mwezi uliopita, kunafanyika huku mashambulizi yikiendelea dhidi ya meli za dawa za kulevya na mvutano wa nchi hiyo na Venezuela ukiendelea kutokota.

Marekani hadi kufikia sasa imetekeleza takriban mashambulizi 19 dhidi ya boti katika visiwa vya Caribbean na mashariki mwa Pasifiki, na kusababisha vifo vya takriban watu 76.

Rais wa Venezuela Nicolas Maduro na maafisa wengine wa Venezuela wameishutumu Marekani kwa "kujitengenezea" mgogoro na kutaka kuiangusha serikali ya mrengo wa kushoto ya kisoshalisti.

Hatua za kuwasili kwa meli ya kivita pia kunawadia huku kukiwa na mvutano kati ya utawala wa Trump na serikali ya Colombia ya Rais Gustavo Petro, ambaye Trump amemtaja kama "jambazi na mtu mbaya".

Petro siku ya Jumanne aliamuru vikosi vya usalama vya umma vya nchi yake kusimamisha ushirikiano wa kijasusi na mashirika ya Marekani hadi mashambulio ya meli katika visiwa vya Caribbean yatakapokoma.

Aliandika kwenye mtandao wa X kwamba mapambano dhidi ya madawa ya kulevya "lazima yawe chini ya haki za binadamu za watu wa Caribbean".

Mapema mwezi wa Novemba, Trump alipuuza uvumi kwamba alikuwa akipanga kupindua serikali ya Venezuela au kuanzisha vita.

Katika mahojiano na CBS - mshirika wa BBC wa habari wa Marekani - Trump alisema kwamba "kila meli moja unayoona imelipuliwa inaua watu 25,000 kwa madawa ya kulevya na kuharibu familia kote nchini."

Hakuna maoni: