Breaking

Alhamisi, 4 Desemba 2025

DC MPOGOLO ATOA WITO WA USHIRIKIANO KWA MADIWANI WAPYA WA JIJI LA DAR


Mkuu wa Wilaya ya Ilala Edward Mpogolo ametoa wito kwa madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kuimarisha umoja na mshikamano ili kufikia malengo ya maendeleo ya jiji hilo. Ametoa kauli hiyo wakati wa kikao cha kwanza cha baraza la madiwani mara baada ya kuapishwa kwa viongozi hao wapya.

Katika hotuba yake, alisisitiza umuhimu wa madiwani kufanya kazi kwa pamoja bila kujali tofauti za kisiasa, akieleza kuwa ushirikiano wao ndiyo msingi wa kuleta mafanikio katika utekelezaji wa miradi ya kijamii na kiuchumi. Aliongeza kuwa malengo ya jiji hayawezi kufikiwa bila kuwepo kwa mazingira ya amani na utulivu ndani ya baraza.

Kiongozi huyo alitumia nafasi hiyo pia kuwapongeza madiwani wapya kwa kupata dhamana ya wananchi na kuwataka kuhakikisha wanakuwa karibu na wananchi katika kushughulikia changamoto zinazowakabili. Alisema wananchi wanategemea uwajibikaji, uwazi na utendaji bora kutoka kwa wawakilishi wao.

Aidha, aliwataka madiwani hao kushirikiana kwa karibu na wabunge pamoja na watendaji wa jiji ili kuhakikisha miradi yote iliyopangwa inatekelezwa kwa ufanisi. Alisisitiza kuwa ushirikiano wa viongozi wote wa maeneo mbalimbali ni muhimu katika kuharakisha maendeleo na kuboresha huduma kwa wananchi wa Dar es Salaam.

Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam inaundwa na kata 36 pamoja na majimbo manne, ambayo yanaongozwa na wabunge kutoka vyama mbalimbali vya siasa. Kupitia umoja wa viongozi hawa, jiji linatarajiwa kusonga mbele katika kufanikisha ajenda zake za maendeleo.

Hakuna maoni: