Breaking

Jumatano, 17 Desemba 2025

MWENYEKITI WA BODI YA WAKURUGENZI TANESCO AKABIDHIWA RASMI OFISI


Mwenyekiti  wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Bw. Plasduce Mbossa, Desemba 16, 2025 amekabidhiwa rasmi ofisi na aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi hiyo,  Mhe. Dkt. Rhimo Nyansaho, ambaye kwa sasa ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.

Hafla hiyo ya makabidhiano imefanyika jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi pamoja na Menejimenti ya TANESCO.

Akizungumza katika hafla hiyo, Bw. Mbossa amesema Mheshimiwa Nyansaho ameondoka akiiacha  TANESCO katika mwelekeo mzuri  na usimamizi mzuri baada ya miradi mingi mikubwa ya umeme kukamilika ikiwemo miradi ya kimkakati kama Bwawa la Kuzalisha Umeme la Julius Nyerere ambalo limechangia kwa kiasi kikubwa kuimarisha uzalishaji na upatikanaji wa umeme nchini.

Aidha, Bw. Mbossa  amepongeza jitihada zinazofanywa katika kuboresha huduma kwa wateja, ambazo zimeongeza ufanisi na kumfanya mteja kuwa kipaumbele.

‘’TANESCO ipo katika mweleko mzuri miradi mingi ya umeme imekamilika na kupelekea nchi kuwa na umeme wa kutosha. Tutaendelea kufanya jitihada za kuongeza uzalishaji wa umeme ili kuendana na kasi ya ongezeko la mahitaji ya umeme,‘’ alifafanua Bw. Mbossa.

Kwa upande wake, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kulinda Taifa ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi aliyemaliza muda wake, Mhe. Dkt. Rhimo Nyansaho, amewashukuru wajumbe wa Bodi na Menejimenti ya TANESCO kwa ushirikiano waliouonesha katika kipindi chote cha uongozi wake ambapo pia amemuahakikisha Mwenyekiti wa Bodi kuwa Bodi  iko imara na anaimani ataendeleza pale alipoishia.

‘’Kwa dhati naishukuru sana Bodi ya Wakurugenzi na Menejimenti ya TANESCO kwa ushirikiano mlionipatia katika kipindi chote tulichokuwa pamoja. Tulishirikiana kwa karibu kutatua changamoto na kuhakikisha Shirika linasonga mbele katika kuwahudumia wananchi,’’ alisema Dkt Nyansaho.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Naibu Mkurugenzi Mtendaji (Uzalishaji), Mhandisi Antony Mbushi, amemshukuru Mwenyekiti  wa bodi aliyemaliza muda wake kwa uongozi na ushirikiano wake mzuri, na kusisitiza kuwa Menejimenti itaendelea kusikiliza na kutekeleza maelekezo ya Mwenyekiti  wa Bodi wa sasa kwa maslahi ya Shirika na Taifa kwa ujumla.

Wakati wa uongozi wake Mhe. Nyansaho alisimamia utekelezaji wa miradi mingi ya umeme na kuhakikisha imekamilika, ikiwemo Miradi ya Bwawa la kufua umeme la Julius Nyerere, Rusumo, Mradi wa kusafirisha umeme wa Lemuguru, Miradi mbalimbali ya Gridi imara, Kuingiza mikoa ya Kigoma na Katavi kwenye Gridi ya taifa na huku akiicha miradi mingine ikiwa katika hatua nzuri za utekelezaji kama Mradi Umeme wa Jua wa Kishapu, ambao mpaka sasa umefikia zaidi ya asilimia 84 ya utekelezaji.

Pia katika kipindi chake, TANESCO imefanikiwa kuboresha mazingira ya kazi kwa wafanyakazi wake jambo lililochangia kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya Shirika pamoja na maboresho makubwa ya eneo la huduma kwa wateja ikiwemo maboresho ya kituo cha miito ya simu, uwepo wa namba 180 ya huduma kwa wateja na mfumo wa Jisoti kuimarisha mawasiliano. 

Hakuna maoni: