Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema kuwa vitendo vya udhalilishaji ni janga la kidunia linalohitaji ushirikiano wa wadau wote ili kuhakikisha linatokomezwa kabisa.
Akizungumza tarehe 07 Disemba 2025, katika hafla maalum ya Msimu wa Tano wa Tuzo za Kupinga Ukatili wa Kijinsia iliyofanyika katika Hoteli ya Madinat Al Bahr, Mbweni, Mkoa wa Mjini Magharibi, Rais Dkt. Mwinyi amesisitiza umuhimu wa wadau na taasisi zinazopinga ukatili wa kijinsia kuungana na kuongeza kasi ya mapambano dhidi ya udhalilishaji, sambamba na kuacha muhali katika kushughulikia matukio hayo.
Ameitaka jamii kutumia maarifa, tafiti na uzoefu uliopatikana katika maadhimisho ya Siku 16 za Kupinga Udhalilishaji kama nyenzo ya kuimarisha juhudi za kukabiliana na vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa ufanisi zaidi.
Aidha, ameeleza kuwa changamoto ya kubadilika kwa jamii na tatizo la baadhi ya wadau kukosa utayari katika kushughulikia kesi za udhalilishaji ni miongoni mwa vikwazo vinavyochelewesha kupatikana kwa suluhisho. Hivyo, amesisitiza umuhimu wa kujenga utamaduni wa uwajibikaji na ushirikiano.
Katika hatua nyingine, Rais Dkt. Mwinyi ameziagiza taasisi za umma kutoa ushirikiano mkubwa kwa Zanzibar Female Lawyers Association (ZAFELA) ili juhudi za kupinga ukatili wa kijinsia ziendelee kwa kasi, akisisitiza kaulimbiu kuwa “Zanzibar bila ukatili wa kijinsia inawezekana.”
Ameipongeza ZAFELA kwa kazi kubwa na mchango wao katika kupinga vitendo vya udhalilishaji, na ameahidi kuwa Serikali itaendeleza ushirikiano nao. Vilevile, amewahimiza washindi wa Tuzo za Kupinga Udhalilishaji mwaka huu kuendelea kutekeleza majukumu yao, akisema mchango wao bado unahitajika zaidi.
Katika hafla hiyo, Rais Dkt. Mwinyi ametunukiwa Tuzo Maalum na ZAFELA kama kutambua mchango wake mkubwa katika kukuza juhudi za kupunguza na kuondoa ukatili wa kijinsia nchini.
Ametoa wito kwa wadau na washirika wa maendeleo kuendelea kuiunga mkono ZAFELA kwa misaada, vifaa na rasilimali mbalimbali ili harakati za kupinga udhalilishaji ziwe endelevu na zenye matokeo chanya.








Hakuna maoni:
Chapisha Maoni