Breaking

Ijumaa, 19 Desemba 2025

TRA YAITEMBELEA KAMPUNI YA SIMBA TRAILERS KUTOA SHUKRANI NA KUIMARISHA USHIRIKIANO.


Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) leo imetembelea Kampuni ya Simba Trailers, inayojihusisha na usafirishaji wa mizigo ya transit, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho mwezi wa Shukrani kwa Walipakodi, kwa lengo la kutoa shukrani na kuimarisha ushirikiano kati ya TRA na walipakodi.

Ziara hiyo iliongozwa na Naibu Kamishna wa Forodha, Bw. Felix Tinkasimile, kwa niaba ya Kamishna wa Forodha, ambapo TRA iliipongeza Kampuni ya Simba Trailers kwa ushirikiano wao mzuri na wa kuaminika katika utekelezaji wa majukumu ya forodha na katika kusaidia ukusanyaji wa mapato ya Serikali.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Naibu Kamishna wa Forodha alisema kuwa Wiki ya Huduma kwa Walipakodi inalenga kuimarisha mawasiliano ya moja kwa moja kati ya TRA na walipakodi, kusikiliza changamoto zao, kutoa elimu ya kodi, na kujenga mahusiano ya kudumu yanayozingatia uwazi, uaminifu na uwajibikaji wa pande zote.

TRA ilisisitiza kuwa wasafirishaji wa mizigo ya transit ni wadau muhimu katika kukuza biashara ya kikanda na kimataifa kupitia korido za usafirishaji za Tanzania, na kwamba ufanisi wao una mchango mkubwa katika kuimarisha ushindani wa Bandari na uchumi wa taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Simba Trailers na mfanyabiashara maarufu nchini, Bw. Azim Dewji, aliipongeza TRA kwa maboresho makubwa yaliyofanyika katika mazingira ya ulipaji kodi, akisema hatua hizo zimepunguza changamoto kwa wafanyabiashara na kuimarisha mahusiano kati ya Serikali na sekta binafsi.

Bw. Dewji alisisitiza kuwa ukusanyaji wa kodi hauwezi kufanikiwa bila kuwepo kwa wafanyabiashara, na kwamba mazingira rafiki na yenye haki ya ulipaji kodi ni msingi wa maendeleo ya uchumi. Aidha, alipendekeza kuimarishwa kwa majadiliano ya mara kwa mara kati ya TRA na wasafirishaji wa mizigo ya transit ili kuboresha mifumo na taratibu za kikodi.

Akihitimisha, Bw. Dewji aliwataka Watanzania kuendelea kulinda amani ya nchi, akisisitiza kuwa amani ndiyo nguzo kuu ya uwekezaji na maendeleo ya taifa.

TRA inaendelea kuwahakikishia walipakodi wote dhamira yake ya kuendelea kuboresha huduma zake, kutoa elimu ya kodi, na kushirikiana kwa karibu na wadau ili kujenga mazingira rafiki ya biashara na kukuza uchumi wa taifa.

Hakuna maoni: